Askofu Mkuu Nkwande: “Mahangaiko na taharuki! Watu hawajui, hivi Tanzania tuliyokuwa nayo tutaendelea kuwa nayo?”
Butiku: “Tumalize Uchaguzi Mkuu, tuanze mchakato wa Katiba mpya huku tukijadili hali ilivyo nchini kwa sasa.”
Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki Mwanza, Renatus Nkwande, anaitafsiri hali ilivyo nchini kwa sasa kuwa ni ‘mahangaiko na taharuki’; huku Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, akitoa wito kwa wananchi ‘kujipanga’.
Akizungumza wakati wa mazishi ya Mzee Silvin Mongella; baba mzazi wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, John Mongella, Askofu Mkuu Nkwande amesema hivi sasa watu wanaogopana kutokana na kuwapo vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.
Anasema hata naye amekumbana na tukio la kutia hofu pale gari alilokuwamo lilipokimbizwa na gari jingine bila kujua nia hasa ilikuwa nini.
“Nimekimbizwa na hizi gari wanazo wakubwa wetu; ‘DFP’. Sijui imeandikwa ‘ziro ziro’ ngapi! Ilikuwa usiku. Tuliposimama tuipishe iende, nayo ikakaa (ikasimama) pembeni. Nikajiuliza, hawa ni watu wa aina gani? Tukaendelea kwenda, wao wanatukimbiza nyuma.
“Tulipopunguza mwendo, tukakaa naye sambamba. Inawezekana alikuwa mhuni, lakini kama haya yanatokea, tunaanza kuwa na wasiwasi!
“Mahangaiko na taharuki iliyopo, ipo. Watu hawajui hivi Tanzania tuliyokuwa nayo tutaendelea kuwa nayo? Tuko katika mahangaiko, tunayoyaona kwenye mitandao; vijana wanasema hadi wakati mwingine wanatukana, siyo ishara nzuri kumtukana mkubwa wako anayaweza kukuzaa,” anasema.
Askofu Mkuu Nkwande anatoa wito wa kuwapo kwa mjadala kuzungumzia namna ya kuyamaliza haya akiamini kwamba hayawezi kumalizika kwa kuzomeana au kubezana.

Anawaomba Watanzania kuzungumza na kutafuta sababu ya kwa nini taifa limefika hapa na ni kitu gani kimelifikisha?
“Kuna padri alizungumza sijui aliona wapi mchungaji ana mabodigadi 20 karibu 30! Pengine huyo mchungaji amenusa shida.
“Mimi sijafika huko, kwa sababu ninajikabidhi kwa Mungu. Ni yeye atakayenilinda usiku na mchana, akiamua kuniacha basi!” anasema.
Amewataka waliopewa dhamana ya kuwalinda Watanzania kutafuta fursa ya kuliunganisha taifa kuzungumzia taharuki iliyopo kwa utaratibu.
Askofu Mkuu Nkwande anasema haitakuwa sahihi pale kila atakayetoa hoja atake tatizo lake ndilo lisikilizwe kwanza, akisema hiyo haiwezekani.
“Tuzungumze. Kila mara huwa nawaambia, hapa tulipo si padogo, huko tulikotoka watu walijipaka grisi badala ya mafuta! Msione leo kina mama wanapendeza,” anasema.
Huenda taharuki na mahangaiko anayozungumzia Askofu Mkuu Nkwande yametokana na tukio la kushambuliwa na kuumizwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maskofu Katoliki, Padri Dk. Charles Kitima, mwishoni mwa Mei mwaka huu, akiwa ndani ya ‘ngome’ ya TEC, Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia ‘taharuki’ hiyo, Paroko wa Parokia ya Mt. Theresia wa Mtoto Yesu Mbezi Luis, Padri Vivian Menezes (OCD), amewataka waamini kuwa walinzi wa wenzao.
“Si mtu anakuja kanisani, unakaa naye, mara anatoka kuzungumza na simu, anarudi; anatoka tena na wewe hauchukui hatua yoyote.
“Chukua hatua. Toa taarifa kwa Kamati ya Ulinzi. Hauwezi kujua labda anataka kumteka Paroko! Tubadilike, wenzetu wamebadilika,” amesema Padri Menezes akitoa mfano wa parokia moja alikokwenda na kukuta ukaguzi na upekuzi wa hali ya juu milangoni.
Butiku na Katiba mpya
Kwa upande wake Mzee Butiku anawataka Watanzania, pamoja na kujadiliana kuhusu hali ya sasa kitaifa, kujipanga na kumaliza shughuli muhimu iliyopo mbele kwa sasa, Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na JAMHURI, Butiku amesema umefika wakati sasa kwa Watanzania kutulia na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.

“Baada ya hapo tuhamie kwenye suala la Katiba mpya. Hili lichukuliwe kwa uzito wa aina yake na kwa haraka,” amesema.
Amesema mchakato wa kupata Katiba mpya ulianzwa wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, ukakwama, lakini Katiba imeendelea kudaiwa, vyama vya upinzani vikiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ).
Mzee Butiku anaamini kuwa ni jambo jema kwa sasa ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeliingiza suala la Katiba mpya kwenye Ilani yake ya Uchaguzi 2025 – 30.
“Nasisitiza, baada ya Uchaguzi Mkuu ujao, tushughulike na ajenda ya kupata Katiba na tuikamilishe haraka. Tusiende nayo mbali sana kwani itaendelea kutuletea shida,” anasema.
Kwa kuwa mchakato wa Katiba mpya ulishawahi kufanyika, Butiku anasema ni muhimu kujadili na kuamua kurekebisha yaliyofikiwa na Bunge Maalumu la Katiba au kuanza upya mchakato mzima.
Amesema kuwamo kwa Katiba kwenye Ilani ya CCM kunaonyesha nia njema ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa taifa.
Mchakato huo ulisimama wakati wa utawala wa Rais John Magufuli, akisema kipaumbele chake ni kushughulikia uchumi.
“CCM imeweka Katiba mpya katika mipango yetu ya taifa (kwa miaka mitano ijayo). Wale wote wanaofikiria hili ni vizuri wakaanza sasa kutoa maoni.
“Naamini (baadaye) serikali itakuja kuweka utaratibu, lakini kila mmoja wetu aanze kufikiria. Tuseme tuwe na mawazo kwamba iko nafasi ya kutengeneza au kupata Katiba mpya.
“Tuwekewe utaratibu wa kushughulikia jambo hilo au tuiombe serikali na chama, baada tu ya uchaguzi kumalizika, watuwekee utaratibu wa jambo hili ili katika kipindi hiki cha miaka mitano basi tulishughulikie,” anasema.
Kuhusu matukio mbalimbali yanayojitokeza nchini kwa sasa, Butiku anaungana na Askofu Mkuu Nkwande, akisema ni muhimu ukapatikana ufumbuzi mapema.
“Kuna mawili. Mosi, hali ya nchi yetu sasa hivi wote tunaifahamu. Ukisikiliza vyombo vya habari na mitandaoni, unaona mambo yalivyo hayawaridhishi Watanzania. hayawapendezi. Tumeyazungumza vya kutosha, tunayafahamu.
“Pili, naomba sasa tuachane na malumbano haya; tujiandae na uchaguzi. Tupate viongozi katika ngazi zote, tutie nguvu pale na kama kuna kasoro tusahihishane ili tupige kura kwa utulivu.
“Sasa baada ya hapo, eeh, ndiyo tushughulike na tuzungumze ajenda mbili tu; hali ya taifa letu kama tunavyoiona sasa na kama tutakavyoina baada ya uchaguzi, na tuzungumze Katiba mpya,” amesema.
Mzee Butiku anasema baada ya kuyakamilisha hayo mawili ndipo taifa litakaposonga mbele huku Watanzania wote wakiwa wameelewana na wanajua wanachokitaka.
“Matatizo hatuwezi kuyaondoa sasa, tumeyasema vya kutosha na wale wanaochocheachochea, nadhani tuache, tutazame uchaguzi, tumalize, tuzungumzie nchi yetu, tumalize tuone kama hayo yote ambayo tunakubaliana tunaweza kuyaweka katika Katiba mpya kama ambavyo CCM ilivyotupatia nafasi,” amesema.
Ends