Na Ruja Masewa, JamhuriMedia, Mbeya
Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Tulia Ackson ameyataka Makundi Maalam yanayokopeshwa Mikopo ya fedha za asilimia 10% za kuwasaidia, Kurejesha marejesho hayo kwa wakati muafaka ili na wengine wakopeshwe.
Tulia ambaye ameongoza kwenye Kura za Maoni za Watiania wa Jimbo la Uyole uliofanyika Agosti 5, 2025 alisema hayo alipokuwa akikabidhi Magari Sita ya kusombea takataka katika jiji la Mbeya kwa Vikundi 5 vya vijana na kimoja cha kina mama kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Hasanga.

Akizungumza baada ya kupokea risala ya Makundi hayo na kuwashukuru kwa kumpa kura za kishindo, Tulia aliyataka makundi yaliyopata mikopo hiyo kurejesha marejesho kwa wakati ili na vikundi vingine viweze kunufaishwa kwa kukopeshwa.
Alisema Hatua hiyo licha ya kuliweka Jiji la Mbeya katika hali ya usafi na mazingira mazuri, pia litaongeza ajira kwa makundi hayo na watu mbalimbali wenye utalaam katika sekta hiyo.
Aidha amewapongeza Watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Justice Kijazi kwa kukusanya Kodi vizuri na kwa Uadilifu mkubwa ambapo umepelekea kupatikana kwa fedha za mikopo hiyo iliyoibua mafanikiyo hayo.
Hata hivyo Tulia aliyataka makundi hayo yatumie mapato na fursa watakayopata kuongeza magari mengi badala ya kurudi kwa mkurugenzi kukopa tena, ambapo aliwaomba Watalaam kuvitambulisha vikundi hivyo kwenye taasisi za fedha pindi wakifanya vizuri, wakitumia Mtaji, Amana na Mafanikiyo Waliyonayo mkononi.

Kuhusu uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, Tulia alichomekea jambo kwa mahasimu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wapinzani akidai,
“Kwa mafanikio haya mliyopata, wale watu watakapokuja wasiwadanganye nanyi mkadanganyika. Kwa maendeleo haya wajibu wetu ni KUTIKI (✔️ ) kwa Rais Samia Suluhu Hassan”.aliyaasa makundi hayo.
Tulia aliwakumbusha, awali Rais Samia alisitisha asilimia hizo 10% kwa makundi maalum kwa sababu kulikuwa na madudu, sintofamu na harufu mbaya, lakini sasa ameiondoa na kuweka sawa na ndiyo maana ya fursa hii.
Miongoni mwa viongozi wa CCM na Serikali waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Solomon Itunda, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Justice Kijazi, Afisa Tawala aliyemwakilisha Katibu Tawala Devota Chacha na Afisa Maendeleo ya Jamii Deus Muhoja.
