Tume ya Madini imeendelea kunadi fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya madini kupitia ushiriki wake kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la Tume ya Madini, Afisa kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Bw. Ashen Mwambage, amesema kuwa sekta ya madini nchini imejaa fursa lukuki zikiwemo utafutaji na uchimbaji wa madini, uanzishaji wa viwanda vya uongezaji thamani madini, biashara ya madini, pamoja na usambazaji wa vifaa na huduma kwenye migodi.

“Tume ya Madini inawakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kushirikiana nasi katika kuendeleza sekta hii kwa kushiriki katika maeneo mbalimbali ikiwemo ubia katika baadhi ya leseni za madini,” ameema Mwambage.
Aidha, ametumia fursa ya maonesho hayo kuhamasisha jamii kujitokeza kupata elimu kuhusu sekta ya madini pamoja na kuelewa jinsi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli zinazochochea maendeleo ya uchumi wa taifa kupitia rasilimali madini.
Tume ya Madini imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa sekta ya madini nchini huku ikijizatiti kuvutia wawekezaji zaidi ili kuchochea ukuaji wa pato la taifa na kuinua maisha ya wananchi.


