📍 Butiama, Mara

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imehimiza kuhusu uhifadhi wa mto Mara ili Kuuwezesha kudumu na kuwa endelevu

Hayo yamejiri wakati wataalamu wa Tume wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi wa Mkoa wa Mara, katika Maadhimisho ya Siku ya Mto Mara (Mara Day), yanayofanyika kuanzia Septemba 12 hadi 15 mwaka huu kwenye Viwanja vya Mwenge, Wilaya ya Butiama, Mkoa wa Mara.

Katika maadhimisho hayo, Tume pia inatoa elimu kwa wananchi kuhusu Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji, ada ya huduma za umwagiliaji na teknolojia za kisasa za umwagiliaji, sambamba na kusisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji.

Mto Mara ni kiunganishi kinachosaidia ustawi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania na Maasai Mara nchini Kenya, ambapo kila mwaka mamilioni ya wanyama wahamao hupita katika eneo hilo, ikiwa ni urithi wa dunia unaotegemea uhai wa bonde hilo.

Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Mara, Mhandisi Adelialidy Mwesiga, amesema miongoni mwa jitihada zinazotekelezwa na Serikali kupitia Tume katika kulinda chanzo cha Mto Mara ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ikiwemo uchimbaji wa visima, ujenzi wa mabwawa na uendelezaji wa Bonde la Bugwema.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo utasaidia kuwaondoa wakulima wanaolima kando ya Mto Mara na kuhamia katika maeneo yenye miundombinu ya umwagiliaji ili kuepusha uharibifu wa chanzo cha maji.

Mara Day huazimishwa kila mwaka Septemba 15 kwa kupokezana kati ya Tanzania na Kenya, ikiwa ni jukwaa la kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa rasilimali maji, uhifadhi wa mazingira na kulinda maisha ya jamii zinazotegemea Bonde la Mto Mara.