Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

TUME ya TEHAMA inaendelea kupanua wigo wa kukuza ubunifu na kuendeleza sekta ya TEHAMA nchini, baada ya kuingia makubaliano na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ya kuendeleza teknolojia katika vyuo saba vya VETA vya wilaya kwa kipindi cha miaka mitano.


Makubaliano hayo yalifikiwa kwa kusaini mikataba ya ushirikiano, kila upande ukisaini mikataba hiyo kupitia Wakurugenzi wake wakuu, Dkt. Nkundwe Mwasaga wa Tume ya TEHAMA na CPA Anthony Kasore wa VETA.

Akizungumza wakati wa tukio huko, Dkt. Mwasaga alisema kazi ya tume yake katika mkataba huo itakuwa ni pamoja na kuweka vifaa vya TEHAMA katika karakana za vyuo hivyo.

Alifafanua kuwa, inawajibika kufanya hilo na mengine, kwa kuwa moja ya majukumu ya Tume yake ni kuendeleza TEHAMA ambapo vijana ndio fursa yao kuingia na kuonesha ubunifu kupitia sekta ya TEHAMA.

Naye CPA Kasore alisema Tume ya TEHAMA itasaidia katika kuongeza ujuzi katika masuala ya Teknolojia kwenye vyuo vya VETA.

Aliongeza kuwa, suala la Teknolojia linakuwa kila siku hivyo ni fursa ya vijana kupata ujuzi wa teknolojia ya TEHAMA kabla ya kuingia katika soko la ajira.

Amevitaja vyuo saba vitavyonufaika na makubaliano ya mafunzo ya TEHAMA ni katika Wilaya za Mpanda, Singida, Njombe, Morogoro, Songea, Mpanda pamoja na Singida.