Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (I-NEC) imevihakikishia vyama vya siasa vyote vitakavyoshiriki uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwezi Oktoba mwaka huu kuwa vitatendewa haki sawa.

Hayo yamebainishwa jana na Kamishna wa Tume hiyo Magdalena Rwebangira alipokuwa akifungua mafunzo ya siku 3 kwa Waratibu, Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo kutoka Mikoa ya Tabora na Kigoma yanayofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha SAUT Mjini Tabora.

Amesema kuwa Tume imeleta mafunzo hayo ili kuwaandaa vizuri waratibu, wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kamishna amesisitiza kuwa Tume imejipanga vizuri ili kuhakikisha taratibu zote za kikatiba na kisheria zinazingatiwa na kufuatwa na wote waliopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi huo ili kuhakikisha unakuwa na ufanisi mkubwa.

Amewataka washiriki wa mafunzo hayo kusoma kwa umakini katiba, sheria, kanuni, miongozo na melekezo yote yanayotolewa na Tume ili kuwarahisishia utekelezaji jukumu hilo na kuepusha malalamiko na vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi.

‘Shirikisheni vyama vya siasa vyote vitakavyoshiriki uchaguzi katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi huo, hakikisheni kanuni, taratibu, sheria, miongozo na maelekezo yote ya tume yanazingatiwa ili kuepusha malalamiko’, amesema.

Aidha amewataka kushirikisha wadau wanaostahili katika maeneo ambayo Tume imeelekeza na kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalumu vya vituo husika ili uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu.

Kuhusu ajira za watendaji wa vituo vya kupigia kura, Kamishna amewataka kutoingiza watu wasio na sifa kwa kigezo cha undugu au jamaa bali wazingatie weledi, uzalendo, uadilifu na uchapa kazi.

Amewataka kukagua na kuhakiki vifaa vya uchaguzi wanavyopokea na kuvisambaza katika maeneo husika kwa wakati, kutoa taarifa wakati wa kuapisha mawakala na kuhakikisha vyama vinapewa orodha ya vituo vya kupigia kura ili viweze kupanga mawakala wao vizuri.

Akiongea kwa niaba ya Washiriki wenzake, Msimamizi wa Uchaguzi wa Manispaa ya Tabora Paschal Matagi ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa kuwa yatawasaidia kufanikisha jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa.