Na Festo Polea

TUME ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, Leo Februari 28 imekutana na mmiliki wa mabasi ya Esther, Joseph Didas. 

Mahojiano hayo ya Tume na Didas yamefanyika katika Ofisi za Tume hiyo zilizopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini hapa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tume kukusanya taarifa, maoni na ushauri kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa sasa, wastaafu.

Katika mkutano huo wa Tume na Didas yamejadiliwa kwa kina namna matukio ya uvunjifu wa amani yalivyoanza, athari zake kwa wananchi, mali zao na miundombinu, pamoja na ushauri na mapendekezo ya namna ya kudhibiti na kuzuia matukio kama hayo yasijirudie siku zijazo.

Hivi karibuni Mamlaka ya Uteuzi imeiongezea Tume muda wa siku arobaini na mbili (42) kuanzia tarehe 20 Februari, 2026 ili Tume iweze kukamilisha uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba, 2025 na kuitaka ikamilishe kazi na kuwasilisha Taarifa yake kabla au ifikapo tarehe 3 Aprili, 2026. 

Kwa sasa Tume inaendelea na mahojiano na waathirika wa Matukio hayo kwa ajili ya hatua zaidi kama Taifa ili Matukio kama hayo yasijirudie tena.