Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya ameushukuru Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kukubali ombi la Mahakama hiyo kuja kujifunza na kusema kwamba wamepata maarifa ya kutosha yatakayowawezesha kutekeleza nchini mwao ili kuboresha huduma za utoaji haki kwa manufaa ya wananchi wa nchi hiyo.

Akizungumza leo tarehe 22 Mei, 2025 katika mahojiano maalum yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Mokaya amesema kuwa, wamepata mapokezi mazuri na kufurahia kila hatua ya ziara yao.

“Tumekamilisha ziara yetu leo, tulianza kwa kutembelea Kituo Jumuishi cha Mahakama Temeke tuliweza kuona jinsi Mahakama hiyo inavyofanya kazi, tuliona pia Mahakama Inayotembea inavyotoa huduma  na vilevile tukaja Dodoma, tumefurahi tumepokelewa vizuri na Jaji Kiongozi, Msajili Mkuu na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania ambao tumekuwa nao muda wote, tunaahidi tutakeleza yote tuliyojifunza,” amesema Mhe. Mokaya.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya akiwa katika moja ya kumbi ya Mahakama iliyopo ndani ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma pindi yeye pamoja na ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya walipotembelea jengo hilo leo tarehe 22 Mei, 2025

Amesema kuwa, yeye pamoja na timu yake wamefurahi kuona jinsi Mahakama ya Tanzania ilivyoboresha huduma zake na kuwa Mahakama ya wananchi yenye miundombinu inayozingatia mahitaji ya wananchi.

“Tumefurahi pia kuona maendeleo makubwa ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ndani ya Mahakama ya Tanzania pamoja na miundombinu mizuri ya majengo ambayo inaonesha kuzingatia na kuthamini utu wa watumishi wake pamoja na wananchi wanaohudumiwa,” ameeleza Msajili Mkuu huyo.

Ameongeza kuwa, Mahakama zote duniani zina changamoto zake, hivyo inahitaji uthubutu katika kufanya mageuzi ya kuboresha huduma na hilo limethibitishwa na Mahakama ya Tanzania na kwamba nao wamejifunza na kuahidi kufanyia kazi yote waliyojifunza.

Kadhalika, Mhe. Mokaya amewakaribisha pia Mahakama ya Tanzania kutembelea Mahakama ya Kenya kujifunza na kubadilishana uzoefu ili kuendelea kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi.

Aidha, ujumbe huo umekutana pia na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ambaye amezungumza nao na kusema nao kuwa, ili Mahakam iweze kufanikiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ni muhimu kushirikiana na mihimili yote ya Dola ikiwa ni Serikali na Bunge.

Katika Siku ya mwisho ya ziara yao , ujumbe huo umetembelea jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na kujionea chumba cha kunyonyeshea Watoto, chumba cha Watoto, ukumbi wa Mahakama (Court room). Vilevile wametembelea jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama lililopo Jirani na jengo la Mahakama.

Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (katikati) akiagana na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya leo tarehe 22 Mei, 2025 baada ya ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya kuhitimisha ziara yao.
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel  (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya na sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania.