Na Kulwa Karedia,Jamhuri Media- Tunduru
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Samia Suluhu Hassan amesema atahakikisha anajenga kituo cha kupoozea umeme katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Amesema kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 116 za ziada ambazo zitatumika kama akiba ili kuhakikisha nishati ya uhakika kwa viwanda vikatavyoanzishwa hasa vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Amesema serikali iko kwenye mchakato wa kufufua viwanda vya kupangua korosho wilayani humo ambavyo vilibinafisishwa na baadae kusitisha shughuli ya uzalishaji wake.
Kama tukifufua viwanda hivi lazima tuwe na ongezeko la uzalishaji umeme, jambo ambalo serikali imelipa kipaumbele ili kuhakikisha viwanda na kongani za mpya vitakavyowekwa vinapata nishati ya kutosha.
Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Wilaya ya Tunduru katika mkutano wake wa kampenzi za uchaguzi mkuu septemba 21, 2025.
Amesema katika ujenzi wa barabara, atahakikisha anakamilisha ujenzi wa barabara Misenjela, Mtwara Mpakani na Rasi Tunduru kwa kiwango cha lami.

Pia kwa kutambua Tunduru kuna wakulima mahiri tumeamua kuzikuza sikimu za umwagiliaji maji,tulileta matrekta 10, mbolea ya ruzuku pamoja na pembejeo, lakini zaidi tumekuza skimu za umwagiliaji, awali zilikuwapo saba, sasa zimefika 21.
Skimu hizo zote zinakwenda kuwasaidia wakulima walime mara mbili kwa mwaka badala ya kusubiri rehema ya mungu ya mara moja kwa mwaka. Juhudi hizi zimesaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Ndani ya wilaya hii kuna ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka 151,944 hadi tani 251,536,amesema.
Amesema kwa mazao ya biashara yameongezeka kutoka tani milioni 31 hadi milioni 42.

Pia ameahidi kujenga soko la kisasa, maghala matatu ya kuhifadhia mazao na kuongeza skimu mbili za umwagiliaji. Kuhusu mifugo amesema wameongeza ruzuku za chanjo, kuongeza majosho, kujenga malambo na mabwawa,kuongeza minada na kuboresha bucha za kuuzia nyama, tumefanya kwa Tanzania nzima.
Jambo la kufurahisha hapa kuna vitalu 221 ambavyo vinasubiri kutumiwa na wafugaji, vingine vimetumiwa na vingine bado tutaleta wawekezaji watumie vitalu hivi ili waongeze uchumi wa wilaya hii.



