Na Manyerere Jackton, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Katika historia ya mabunge ya Tanzania, Bunge la 12 (2020 – 2025) litabaki kuwa moja ya mabunge yaliyozua mijadala mikubwa kuhusu hadhi, majukumu na ushawishi wake halisi katika kuisimamia serikali.
Wapo wanaodiriki kusema kuwa huenda Bunge hili linalomaliza muda wake ndilo Bunge dhaifu katika historia ya mabunge yote ya nchi hii.
Udhaifu wa Bunge hili umedhihiri juzi wakati wabunge wa Bunge hili, kwa maarifa madogo, walipoamua kuwashambulia Wakenya bila kutambua kuwa jukwaa wanalotumia lilihitaji kauli makini zinazobeba diplomasia na utangamano. ‘Vita’ ya aina hiyo inapiganwa na wabunge maalumu, si kila mbunge. Matokeo yake Wakenya wakatushughulikia kweli kweli.
Likiwa na wabunge wa CCM zaidi ya asilimia 95, Bunge hili lilianza kwa mbwembwe nyingi, lakini linamaliza muda wake likikosolewa kwa kuwa dhaifu mno mbele ya mamlaka ya kiutendaji ya serikali.
Bunge hili lilianzishwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 uliolalamikiwa na vyama vya upinzani, mashirika ya kiraia, wachambuzi wa siasa, na hata wana CCM wanaoamini katika haki na kweli. Uchaguzi wa mwaka huo haukuwa uchaguzi, bali kituko tu cha kukarahisha suala hilo la kikatiba.
Waliokuwa wabunge kupitia vyama vya upinzani walishindwa kurejea bungeni, wengine wakihama kwa shinikizo au vishawishi na kujiunga na chama tawala. Mtu yeyote anayelitakia heri taifa letu hawezi kushangilia kuona vyama vya ushindani vikinyongwa na kubaki na chama kimoja.
Wabunge kama Josephat Gwajima, na Luhaga Mpina, wanavyoichachafya serikali ni matokeo ya ‘kunyongwa’ kwa watu waliopaswa kuifanya kazi hiyo, yaani wabunge wa vyama vya upinzani. Asili hairuhusu ombwe. Hauwezi kuua wakosoaji ukitarajia wenzako ulionao hawatabadilika kuziba nafasi hiyo ya ukosoaji. Hiyo ni kanuni ya asili.
Mkandarasi wa hili Bunge ni hayati John Magufuli, akitumia kofia zake mbili za urais na uenyekiti wa CCM. Alihakikisha hata watu ambao ni dhaifu kifikra kwa kuwasikia na kuwatazama, wanaingia bungeni kufanya kazi zinazohitaji weledi.
Kwa mara ya kwanza tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, Bunge limekuwa na upinzani mdogo mno, hali iliyolifanya lionekane wazi kuwa ni chombo cha kupitisha kila kinachotoka serikalini bila kuhoji.

Kila mwaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amekuwa akitoa ripoti nzito kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma, ubadhirifu na upotevu wa mapato. Lakini Bunge limekuwa kimya – hakuna hoja nzito zilizojadiliwa bungeni kutokana na ripoti hizo, hakuna mawaziri waliowajibishwa, na hakuna mabadiliko ya kweli yaliyosukumwa na Kamati za Bunge kama LAAC na PAC.
Mfano, katika ripoti ya CAG ya mwaka 2022/2023, shilingi zaidi ya bilioni 300 zilionekana kuwa na matumizi yenye dosari, lakini hakuna hoja ya dharura iliyoibuliwa bungeni.
Katika kipindi cha miaka mitano, Bunge hili limepitisha au kubariki sheria kadhaa ambazo wachambuzi wanaziita kandamizi. Sheria ya Takwimu, Sheria ya Huduma za Habari, na Sheria ya Makosa ya Mtandao zimeendelea kutumika kama zana za kudhibiti uhuru wa kujieleza, huku wabunge wakiwa kimya au hata wakizitetea.
Lakini Bunge hili hili limepitisha sheria ya mafao ya viongozi na wenza wao. Hili si jambo la kustaajabisha kwa taifa ambalo uchumi wake ni imara na wananchi wanaishi vizuri.
Sheria ya mafao ya viongozi na wenza wao ni miongoni mwa sheria mbaya mno kuwahi kuwapo katika taifa letu. Ni sheria zinazowaumiza wananchi walipakodi. Wananchi hawapingi viongozi wao wastaafu kutunzwa, lakini hiki kilichofanywa na Bunge kinadhihirisha namna tabaka la watawala linavyojitazama wao kuliko hao wanaotawaliwa.
Sote tunatambua kuwa tayari kulishakuwapo sheria za kuwatunza wastaafu hao, lakini kuongeza wigo kwamba sasa wenza wao nao walipwe mafao, ni uonevu kwa Watanzania maskini.
Mwaka 2023 ulipotangazwa mchakato wa kufanya mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa, ilitarajiwa kwamba Bunge lingeongoza mjadala wa kitaifa – lakini badala yake, liliweka kando hoja hiyo kwa visingizio vya kiutaratibu. Matokeo yake yalifanywa mabadiliko ambayo baadhi yanakosolewa.
Wakati wananchi na vyama vya siasa wakipaza sauti kutaka Katiba Mpya, hususan mwaka 2022 na 2023, Bunge halikuchukua nafasi ya kuongoza mchakato huo.
Katika Bunge hili, mijadala mingi imehusu matusi ya kisiasa, vijembe kati ya wabunge, na kejeli dhidi ya vyama vya upinzani. Hoja kama ajira kwa vijana, hali ya elimu, bei ya mafuta na vyakula, na ulinzi wa mazingira zilikosa nafasi ya kina katika mijadala ya Bunge.
Haikushangaza kuona kwa mara ya kwanza bajeti ya wizara ikichangiwa kwa mdomo na mchangiaji mmoja pekee. Bajeti za wizara nyeti kama Maliasili na Utalii ambazo mabunge yaliyopita zilichangiwa kwa siku mbili au hata tatu, kwenye Bunge hili imechangiwa siku moja – tena kwa saa kadhaa.
Katika mfumo wa demokrasia ya uwakilishi, Bunge linapaswa kuwa na meno ya kuhoji, kuwasilisha malalamiko ya wananchi, na kuilazimisha serikali iwajibike. Lakini kwa Bunge hili, wananchi walishuhudia taasisi hiyo ikiweka mbele kusifu serikali kuliko kuitaka iwajibike. Maswali ya msingi ya wananchi hayakupata nafasi ya kufikishwa au kuulizwa bungeni, na hoja za upinzani hazikufikishwa kwa ufasaha.
Bunge hili limediriki kuzima hoja ya kujadili mauaji, kupigwa na kupotezwa kwa watu wa kada mbalimbali nchini, wengi wakiwa ni wale wakosoaji wa serikali.
Maisha ya mwanadamu hayawezi kulinganishwa na kitu chochote. Tumeona Wakenya wanavyoacha mambo yote -kuanzia bungeni hadi mashambani – kujadili kuuawa kwa kijana Ojwang. Sisi hapa watu wanatekwa, wanauawa na wengine wanapotezwa lakini Bunge wala halioni kama ni muhimu kujadili suala hilo.
Kunatokea vifo vya watu zaidi ya 30 katika ajali moja, na baadaye wiki hiyo hiyo wanakufa wengine zaidi ya 10; Bunge wala halishituki! Linaendelea na mijadala ya vijembe na mipasho kana kwamba taifa halina msiba. Kila mwanachi mpenda nchi anawajibika kuhakikisha aina hii ya Bunge inakomea kwenye Bunge hili la 12.
Bunge hili limeacha somo kubwa kwa taifa: kwamba mfumo wa kidemokrasia unaweza kupoteza maana yake iwapo taasisi za uwajibikaji – hasa Bunge – zitageuzwa kuwa matawi au mihuri ya serikali. Taifa linahitaji Bunge lenye meno, lenye heshima, na lenye ujasiri wa kusema “hapana” pale panapostahili.
Mwito kwa Watanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ni mmoja: chagua wabunge wenye uwezo wa kufikiri kwa uhuru, si wapiga makofi wa serikali.
Yawezekana kabisa tunampenda Rais Samia Suluhu Hassan, na kwa namna ilivyo, atashinda uchaguzi ujao. Pamoja na mapenzi makubwa kwake, njia nzuri ya kumsaidia ni kuhakikisha anakuwa na Bunge imara, linaloundwa na wabunge makini.
Chama Cha Mapinduzi kiachane na ile dhana ya kushinda viti vyote vya ubunge na udiwani, badala yake kiwe radhi kuona vyombo hivyo viwili vya uwakilishi vinakuwa na watu wanaokinzana kimitazamo na walio tayari kusaidia kunyoosha mambo ambayo CCM wenyewe hawawezi kuyafanya.
Bunge hilo ili liwepo, hatua kubwa na ya msingi ni kuhakikisha njia za kuwapata wabunge ni zile zilizoainishwa kwenye taratibu za vyama na sheria za nchi.
Bila Bunge madhubuti, rushwa itaota mizizi, haki za wananchi zitakiukwa, na maendeleo ya kweli yatabaki ndoto.
0769 488955