Na Mwavua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Ubalozi wa Japan nchini unatarajia kujenga bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Pangani, Kibaha mkoani Pwani, kwa lengo la kupunguza changamoto ya wanafunzi wa kike kutembea umbali mrefu na kuishi nje ya shule.
Hayo yalielezwa Februari 9, 2026 na mwakilishi kutoka Ubalozi wa Japan, Riho Tokoro, alipotembelea shule hiyo kukagua bweni dogo lililopo pamoja na kisima cha maji na kuzungumza na wanafunzi.
Tokoro alisema mpango wa ujenzi wa bweni hilo upo katika hatua za utekelezaji wa bajeti, unaotarajiwa kuanza Juni mwaka huu.
Alieleza kuwa ubalozi hupokea maombi mengi kutoka mikoa mbalimbali, hivyo watajadiliana na uongozi wa shule na kata ili kubaini kipaumbele kikuu cha changamoto zilizopo na kiwango cha msaada watakaoweza kutoa.
Alifafanua kuwa Ubalozi wa Japan ulianza kutekeleza miradi ya kijamii nchini Tanzania tangu mwaka 1989 kupitia sekta za elimu, afya, kilimo na maji, hadi sasa miradi 389 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 28 imetekelezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Pangani, John Katele, ameushukuru Ubalozi wa Japan kwa kukubali ombi hilo, akisema litasaidia kuondoa kero kwa wanafunzi wa kike wanaolazimika kuishi mbali na shule.
Vilevile, Katele aliishukuru Manispaa ya Kibaha chini ya Dkt. Mkurugenzi Rogers Shemwelekwa kwa kuipatia shule hiyo madawati 150, akisema hatua hiyo inaonesha utekelezaji wa ahadi kwa vitendo na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya elimu ya msingi na sekondari.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Pangani, Tatu Mwambala, alieleza shule hiyo ilianzishwa mwaka 2007 na kwa sasa ina bweni moja lililojengwa mwaka 2013 lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 64 pekee.
Alieleza kuwa shule ina jumla ya wanafunzi wa kike 570, hivyo kuna upungufu wa mabweni sita ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi 506 waliobaki na ukosefu wa bwalo la chakula.
“Bweni lililopo haliwatoshi wanafunzi, Tunahitaji bweni litakalowawezesha watoto kuishi shuleni na kuepukana na changamoto wanazokutana nazo njiani wanapokuja na kuondoka shule,” alisisitiza Mwambala.
Naye Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Kibaha, Theresia Charles, anasema uhitaji wa mabweni ni mkubwa huku manispaa hiyo ikiwa una shule 24 za sekondari za serikali na sita ndizo zenye mabweni na nyingi hupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita.








