Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Jiji la Arusha, moja ya miji muhimu ya kitalii na kibiashara nchini Tanzania, linakabiliwa na changamoto kubwa ya ubovu wa barabara, hasa zile zilizopo katikati ya mji. Barabara nyingi ni nyembamba na hazijaendelezwa kulingana na ongezeko la magari na watu.

Hali hii imepelekea msongamano mkubwa wa magari, ajali na kuchelewesha shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii.

Wakazi wa jiji hili wanapata adha kubwa kutokana na hali duni ya barabara, mashimo yaliyotapakaa barabarani husababisha kero kubwa kwa watumiaji wa barabara pamoja na kuhatarisha usalama wa vyombo vya moto.

Aidha madereva wa bodaboda na bajaji ambao ni tegemeo kubwa la usafiri kwa wakazi wa kipato cha chini hulazimika kutumia njia zisizo rasmi jambo linaloongeza hatari ya ajali.

“Hali hii huchangia kuchelewesha huduma za dharura kama vile ambulansi na magari ya zimamoto, hata baadhi ya maeneo imekuwa vigumu kufika kwa wakati eneo la tukio, hali inayosababisha madhara yanayoweza kuepukika” amesema Elius Mawazo Mkazi wa Ngarenaro.

Wakizungumza na Jamhuri Digital wafanyabiashara wa kati na wadogo wamesema wanaathirika zaidi kutokana na barabara mbovu hali inayoathiri mapato yao ya kila siku na pia kuathiri ukuaji wa biashara ndogondogo ambazo ni mhimili wa uchumi wa Arusha.

“Mizigo huchelewa kufika sokoni au kufika ikiwa imeharibika, kwa mfano wiki iliyopita nilipata hasara ya kreti tatu za soda, zilivunjika baada ya boda kuingia kwenye shimo na kuanguka kwa madai kuwa hakuweza kuliona mapema, kama ni kweli anayosema basi nailaumu serikali kwa kushindwa kufanya marekebisho kwa wakati kwenye barabara zetu wakati tunalipa kodi” amesema mama Samson mfanyabiashara wa Majengo.

Katika jiji lenye fursa kubwa kama Arusha, ubovu wa barabara unahatarisha uwekezaji katika sekta ya utalii. Watalii kutoka nje ya nchi hupitia barabara hizo hizo kuelekea mbuga maarufu kama Serengeti, Manyara, Tarangire na Ngorongoro hukumbana na barabara zisizopitika vizuri hivyo kuleta taswira hasi kwa nchi.

Wadau wa maendeleo wameishauri Serikali kuboresha hali hii kwa kuhakikisha uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya barabara kupitia mamlaka zake kama vile Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuandaa na kutekeleza mipango kabambe ya ujenzi na upanuzi wa barabara kulingana na mahitaji halisi ya jiji na ukuaji wake.

“Hapa kunahitajika uwekezaji wa kimkakati kama vile kuimarisha mifereji ya maji ya mvua ili kuzuia barabara kuharibika wakati wa mvua, kutumia vifaa bora vya ujenzi, na kuajiri wakandarasi wenye sifa na uwajibikaji, vilevile Serikali inapaswa kushirikiana na sekta binafsi katika kuboresha miundombinu kwa kutumia mikataba ya ubia (PPP)” amesema mmoja wa mwekezaji kwenye sekta ya utalii na kuongeza,

“Pia Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya barabara zinasimamiwa ipasavyo ili kuepuka ufujaji na matumizi yasiyo sahihi, kusimamia uwajibikaji wa watendaji wa Serikali katika ngazi zote ili kupata barabara zenye viwango vya ubora wa kimataifa”

Akizungumza na Jamhuri digital ofisini kwake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha Mhandisi Nicholaus Francis amesema zoezi la ukarabati wa barabara zote zenye changamoto wa ubovu litaanza ikiwa ni pamoja na kuweka lami barabara mpya ili kupunguza msongamano uliopo.

“Tuna mpango wa ukarabati wa barabara zetu kubwa na kuweka mifereji, lakini Kwa kushirikiana na wenzetu wa Jiji pamoja na Jeshi la Polisi tuna mpango wa kuhakikisha msongamano ulipo unamalizika kwa kuondoa maegesho ya magari yasiyo rasmi na kuainisha barabara zitakazotumia kwa ajili ya kuingia na kutoka” amesema Mhandisi Francis.

Amesema hadi sasa tayari wameshaainisha barabara kumi ambazo zitatumika kwa njia moja na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutii sheria.

Ili kupata mafanikio ya kweli Serikali inapaswa pia kuangalia mifano ya mafanikio kutoka katika majiji mengine barani Afrika likiwemo Jiji la Kigali nchini Rwanda ambalo kimefanikiwa kuwekeza katika barabara nzuri, safi na zenye mifumo bora ya kuondoa maji ya mvua. Hali hii imesaidia kukuza utalii, biashara na kupunguza ajali.

Vivyo hivyo jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini lina mtandao wa barabara uliopangwa vizuri, wenye njia za magari, watembea kwa miguu na baiskeli. Miundombinu hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuweka jiji hilo salama, safi na la kisasa, hali ambayo huvutia wawekezaji na watalii.

Changamoto ya ubovu wa barabara katika jiji la Arusha ni suala la dharura linalohitaji hatua za haraka na za kimkakati kutoka kwa Serikali. Uwekezaji wa kweli katika miundombinu bora ya barabara sio tu unarahisisha maisha ya kila siku ya wananchi, bali pia ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Serikali inapaswa kuchukua hatua sasa ili kuhakikisha jiji la Arusha linaendana na hadhi yake kama kitovu cha utalii na biashara.