Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Ndugu zangu Watanzania, leo nataka kuandika mada ngumu kidogo. Niseme wazi tu kuwa nimefanya kazi hii ya uandishi kwa miaka 32 sasa. Nimeuona, nimeuandika, na nimeuishi uchaguzi. Nimeshuhudia mabadiliko mengi tangu uchaguzi wa mwaka 1980. Wakati huo tulikuwa na chama kimoja, na mgombea wa urais alikuwa mmoja – akitumia picha ya mgombea na msitu.
Sitanii, katika mfumo ule wa chama kimoja, tulitumia mfumo wa jembe na nyundo au kuku na yai, au nyumba na jembe kwa wagombea ubunge. Kampeni zilipamba moto. Watu walishiriki mikutano na mijadala mizito kuliko maelezo. Nyimbo zilitungwa. Tusisahau kuwa nchi haikuwa na sukari, maji ya bomba, barabara, ndege, hospitali, shule zilikuwa chache, kwa maana darasa la saba anashinda mtoto mmoja katika darasa la watoto 60!
Hata hivyo, bado katika mfumo ule wa chama kimoja, kulikuwa na hamasa kubwa. Wananchi walipanga foleni ndefu, wakijua watatimiza wajibu wao wa uraia wa kupiga kura. Kwa ubunge, ingawa wagombea wote walitoka chama kimoja, bado walitumia alama tofauti kama nilivyosema. Katika Jimbo langu la Bukoba, nakumbuka wagombea Samuel Ntambara Luhangisa na Mwalimu Emmanuel Rugumila, walitumia nyumba na jembe.
Miaka imepita. Tumepiga hatua kubwa – vyama vingi, uhuru wa habari, teknolojia ya kisasa, na wananchi walioelimika zaidi. Lakini kinachonishangaza ni kwamba hamasa ya uchaguzi imeporomoka.
Wapo wanaosema “uchaguzi ni maigizo,” wengine wanadai “matokeo yanajulikana mapema.” Wengine hawataki kabisa kujihusisha na siasa. Wanasema wamechoshwa na ahadi zisizotekelezwa, kero zisizopatiwa majibu, na wanasiasa wanaowakumbuka wananchi tu wakati wa kampeni.
Lakini tukisogea karibu, tutagundua jambo moja: watu hawa wanaoukataa uchaguzi, bado wanauishi kwa ndani. Wanafuatilia kila kinachojiri, wanawajadili wagombea kwenye vibanda vya kahawa, wanachambua mijadala ya kampeni mitandaoni, na wanahoji nani “anaweza kushinda.” Kwa lugha rahisi, wameukataa uchaguzi kwa maneno, lakini mioyoni mwao wanaupenda.
Sasa, swali langu ni hili: kwa nini tunakataa kitu tunachokitamani? Ninaamini Watanzania hawajaichoka demokrasia; wamechoshwa na uongo usioeleza uhalisia wa kinachotendeka. Sisi wakazi wa Mkoa wa Kagera, ilikuwa tukitaka kusafiri kuja Dar es Salaam, ilitulazimu kupita Kampala – Uganda, Busia – Nairobi, Kenya na kurejea nchini kwetu kwa sababu ya ubovu wa barabara.
Sitanii, leo ni tofauti. Tuna barabara nzuri, SGR, ndege na usafiri binafsi kwa kiwango ambacho hakijapata kutokea. Ilikuwa wamechoka kuona kura zao zikibadilika kuwa namba zisizoakisi uhalisia. Kinyume chake, kwa sasa wananchi wamechoshwa na siasa za kejeli badala ya hoja, kampeni za mizaha badala ya mipango ya maendeleo. Wamewachoka wanasiasa wanaotoa hoja bandia.
Lakini hata katika hali hiyo, bado wana ndoto ya kuona uchaguzi wa kweli – wa heshima, wa hoja, na wa haki. Wana hamu ya kuona viongozi wanaoshindana kwa sera, si kwa kebehi. Wana kiu ya kuona kura yao ikihesabiwa na kuheshimiwa. Ndiyo maana, kila uchaguzi unapokaribia, hali ya hewa ya kisiasa hubadilika. Watu huanza kufuatilia, kushiriki mijadala, na kuonyesha hisia.
Tukikumbuka historia, hata wakati wa chama kimoja, wananchi walikuwa na imani na mfumo. Leo tuna uhuru mkubwa zaidi, lakini tuna hofu kuliko wakati ule. Labda tatizo si mfumo, bali imani. Tumepoteza imani kwamba uchaguzi unaweza kuleta mabadiliko.
Uchaguzi ni kioo cha taifa. Nasikia wapo wanaosema hawatashiriki. Walitangaza wazi, ila wanahangaika kila kona. Wanaandika barabarani maandishi, kwenye majengo kuwa hakuna uchaguzi. Sasa kama mliukataa, si msubiri uishe ndipo mtueleze hoja zenu?
Napigiwa simu za kibabe. Kuna watu wanasema Watanzania andamaneni. Tena bila aibu, wanasema nenda muuawe angalau 60 hatua zichukuliwe. Wao wanaotuelekeza hivyo, wako Marekani.
Watanzania, uchaguzi si adui. Ni nafasi ya kutafakari mustakabali wetu. Tatizo ni sisi – tunaukataa kwa sauti bila kujua matatizo ya kuukataa uchaguzi, lakini mioyoni tunautamani. Hivi mkoje? Naomba turudi mezani. Tuwaze kuhusu taifa letu. Amani Kwanza. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404827