Ufaransa na Saudi Arabia zitaongoza mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi na serikali katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kujaribu kufufua matumaini ya suluhisho la mataifa mawili ambayo yalikuwa yamekwama kwa muda mrefu.
Mkutano huo unafanyika mjini New York, Marekani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, katika wakati ambapo shinikizo la kimataifa dhidi ya Israel likiongezeka kutokana na vita vya Gaza.
Katika mkutano huo, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron anatarajiwa kutangaza hatua ya Ufaransa kuitambua rasmi Palestina kama taifa huru.
Nchi nyingine kadhaa za Magharibi, ikiwemo Uingereza, Canada, Ubelgiji, na Australia, zinatarajiwa pia kuchukua hatua hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, Varsen Aghabekian Shahin amesema hatua ya nchi hizo kulitambua taifa huru la Palestina, inaleta karibu zaidi uhuru na mamlaka ya Wapalestina.
