Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
JAMII imeshauriwa kuchangamkia fursa ya ufugaji wa sungura kibiashara kutokana na soko lake linalozidi kukua nchini na faida lukuki za kiafya na kiuchumi zinazotokana na nyama yake na mazao mengine ya sungura.
Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya Saore inayojishughulisha na ufugaji wa sungura, Suleyman Rugarabamu, amesema kampuni hiyo imejipanga kusaidia wananchi kupitia mtaji, teknolojia na soko la uhakika ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Tumeandaa mfumo maalum kwa makundi matatu; wale wasio na mtaji, walio na mtaji na wale wenye majukumu mengi. Tunajenga mabanda, tunatoa sungura wa kuanzia na baadaye tunanunua sungura hao wakishafikia kilo moja. Hii ni fursa ya kila mtu kuongeza kipato na hata kusomesha watoto kupitia kilimo hiki,” amesema Rugarabamu.
Ameongeza kuwa sungura wanaotolewa kwa wafugaji wanakuwa na bima, hivyo iwapo atafariki mfugaji atapatiwa mwingine bure.
Aidha, ameweka wazi faida za ufugaji huo ikiwemo uwezo wa sungura kuzaa watoto 6–16 kwa mara moja na kila mwezi, sambamba na thamani ya mkojo na kinyesi ambacho pia huuzwa kama mbolea.
Kwa upande wake bondia wa ngumi, Karim Mandogo, amesema amejiunga na hamasa hiyo ili kuonyesha mfano kwa vijana wenzake, akisisitiza kuwa ufugaji wa sungura unaweza kugeuka chanzo kipya cha ajira na kipato.

“Vijana jitokezeni kwa wingi, Saore wanatoa sungura kama mtaji na wanajenga banda. Baadaye wao wenyewe wanakuja kuwanunua. Mimi nimepanga kula nyama ya sungura mara kwa mara ili kuimarisha misuli yangu na kuongeza nguvu ulingoni. Hakuna tena bondia wa kunipiga,” amesema.
Kampuni ya Saore ilianza mwaka 2018 na tayari imewafikia zaidi ya watu 6,000 waliokuwa wakifaidika kupitia mfumo wa kifamilia na kirafiki, lakini sasa imefungua rasmi fursa hiyo kwa Watanzania wote.
