Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Uhamiaji Mkoa wa Pwani, imejidhatiti kuimarisha doria na misako, na kuweka maofisa wa uhamiaji katika ngazi ya kata ili kudhibiti raia wanaoingia au kupita mkoani humo bila kuwa na vibali halali.
Hatua hiyo inalenga kuongeza umakini katika ufuatiliaji wa wageni na kurahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu wahamiaji haramu katika ngazi ya jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na matarajio ya idara hiyo, Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Pwani, SACI. Dorah Luoga, aliwasihi raia wa kigeni na wawekezaji kufuata sheria na taratibu za nchi kwa kuhakikisha wanakuwa na vibali halali ili kujiepusha na mkono wa dola.
Alieleza licha ya kuonekana kwa ongezeko la idadi ya wahamiaji haramu waliokamatwa, hali hiyo inaashiria kuimarika kwa udhibiti na si kuongezeka kwa tatizo.
“Mwaka 2024 tulikamata wahamiaji haramu 958, huku mwaka 2025 idadi ikifikia 1,479,;Ongezeko hili limetokana na kuimarishwa kwa doria, misako na ushirikiano wa wananchi, jambo linalosaidia kuwabaini wanaoingia kupitia njia zisizo rasmi mapema na kuchukuliwa hatua za kisheria,” alieleza Luoga.
Alifafanua kuwa lengo la idara si kuongeza idadi ya ukamataji bali kupunguza mianya ya uingiaji haramu kupitia njia za panya.
Kadhalika alibainisha, idara hiyo imeendelea kutoa elimu kwa wananchi, wanafunzi, wamiliki wa nyumba, bodaboda na wenye magari ili wajiepushe kusaidia wahamiaji haramu na kutambua madhara yake.
“Tunawaingiza wageni na wawekezaji kwenye kanzi data maalum inayotambua kibali cha kila mmoja na muda wake wa kuisha, hii inatusaidia kufuatilia kwa karibu na kuchukua hatua pale inapobidi,” alisisitiza.
Luoga pia aliwataka wananchi kuwa walinzi wa amani kwa kutoa taarifa za watu wanaowashuku kuingia katika mitaa na kata zao bila kufuata taratibu za kisheria.
Baadhi ya wakazi wa Ungindoni, Kibaha, akiwemo Godfrey John na Amina Saleh, waliishukuru idara hiyo kwa kusogeza huduma katika ngazi ya kata kupitia watendaji na wenyeviti wa mitaa, wakisema hatua hiyo itarahisisha utoaji wa taarifa na kusaidia kudhibiti wahamiaji haramu kwa haraka.


