Na Lookman Miraji

Taifa la Uingereza huadhimisha siku maarufu nchini humo, ijulikanayo kama siku ya mfalme Charles wa tatu(KING CHARLES III ). Siku hiyo ni miongoni mwa sikukuu za kitaifa nchini humo ikiwa imebeba maana kubwa kwa watu wa taifa hilo.

Siku ya Mfalme Charles III wa Uingereza ni tukio la kitaifa linaloadhimishwa kuenzi kuzaliwa kwa mfalme huyo, ambaye ni mkuu wa nchi ya Uingereza na Jumuiya ya Madola. Ingawa siku yake halisi ya kuzaliwa ni Novemba 14, sherehe rasmi za kitaifa huadhimishwa mwezi Juni, kwa kawaida ili kufaidika na hali nzuri ya hewa.

Siku hii ni zaidi ya kumbukumbu ya kuzaliwa ikiwa pia ni ishara ya uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia kati ya Uingereza na nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.

Katika nchi kama Tanzania, siku hii huadhimishwa kwa hafla maalum katika makazi ya balozi wa Uingereza, kama ilivyofanyika tarehe 18 Juni 2024, ambapo viongozi wa serikali, wanadiplomasia, na wageni mashuhuri hukusanyika kusherehekea tukio hilo kwa heshima ya mfalme.

Tukiirejea historia inatueleza kuwa mahusiano rasmi kati ya Tanzania (hasa Tanganyika kabla ya Muungano) na Uingereza yalianza katika mwaka 1919, baada ya Mkutano wa Amani wa Versailles uliofanyika baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia. Katika mkutano huo, iliamuliwa kuwa Tanganyika iwe chini ya utawala wa Uingereza kama eneo la kudhaminiwa, kwa lengo la kuandaliwa kuelekea uhuru.

Uhusiano huo uliendelea kubadilika kadri miaka ilivyopita, hasa baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, na baadaye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 kuunda Tanzania. Tangu wakati huo, Uingereza imekuwa mshirika wa muda mrefu wa Tanzania katika nyanja za biashara, elimu, afya, na maendeleo.

Mahusiano hayo rasmi kati ya Tanzania na Uingereza ambayo mpaka sasa yameendelea kudumu kwa zaidi ya nusu karne hadi hivi leo. Kupitia mahusiano hayo yameshuhudiwa mafanikio makubwa ya mahusiano hayo hususani katika nyanja mbalimbali.

Hadi kufikia miaka ya hivi karibuni, mahusiano kati ya Tanzania na Uingereza yameimarika kwa kiasi kikubwa, hasa katika nyanja za biashara, uwekezaji, na nishati.

Mosi, kwa kuthibitisha hayo yote itakumbukwa mnamo mwaka 2024 Tanzania na Uingereza ziliingia katika Mkataba wa Ushirikiano wa Ufanisi wa Pamoja (MPP). Tanzania na Uingereza zilisaini mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya takribani Shilingi trilioni 3.2 (sawa na Pauni bilioni 1). Mkataba uliolenga kuchochea maendeleo katika sekta za biashara, uwekezaji, afya, miundombinu, na jamii.

Eneo jingine la ushirikiano baina ya serikali ya Tanzania na Uingereza ni katika sekta ya nishati. Katika sekta hii Uingereza imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya nishati nchini Tanzania, ikiwemo kupitia taasisi zake kama UK Export Finance (UKEF) na British International Investment (BII). Mfano mzuri wa ushirikiano katika sekta hii ni ufadhili wa zaidi ya Shilingi bilioni 11 kwa miradi kama Songas, pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mbali na maeneo hayo mawili eneo jingine la ushirikiano baina ya Tanzania na Uingereza ni kupitia Uwekezaji wa moja kwa moja wa Uingereza.(Foreign Direct Investment). Katika eneo hilo muhimu la kiuchumi, kupitia Kampuni kama Serengeti Breweries Limited (SBL), inayomilikiwa na Diageo ya Uingereza, imekuwa mfano wa uwekezaji unaowajibika. Aidha pia SBL imekuwa ikisaidia wakulima wa ndani, kutoa ajira, na kuchangia maendeleo ya jamii kupitia miradi ya maji safi na mafunzo ya ujuzi.

Kwa ujumla, mwelekeo wa sasa unaonyesha dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii, huku Uingereza ikionekana kuwa mshirika wa karibu katika safari ya maendeleo ya Tanzania.

Katika kuadhimisha siku ya mfalme Charles wa tatu wa Uingereza kwa mwaka huu 2025, Hapa nchini siku hiyo imeadhimishwa kwa hafla maalum katika makazi rasmi ya balozi wa Uingereza nchini ambapo iliwaleta pamoja viongozi wa serikali, wanadiplomasia na wageni wengine mashuhuri kusheherekea tukio hilo kwa heshima ya mfalme.

Katika hafla hiyo, Mbali na viongozi waandamizi kutoka wizara ya mambo ya nnje na ushirikiano wa Afrika mashariki waliohudhuria tukio hilo, Mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa nchi, ofisi ya Rais, mipango na uwezekezaji, Prof: Kitila Mkumbo(Mb).

Akizungumza katika maadhimisho ya siku hiyo, Prof:Mkumbo ameishukru serikali ya Uingereza kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa Tanzania katika sekta mbalimbali.

Aidha Waziri Mkumbo ameelezea kuhusu dhamira ya serikali katika kuendelea kuvutia wawekezaji nchini ikiwa ni sehemu mojawapo pia ya kutekeleza kwa vitendo dhana ya diplomasia ya uchumi(Economic diplomacy) ambayo imekuwa ni kipaumbele muhimu cha sera mpya ya mambo ya nnje.

Mbali na hayo, Balozi wa Uingereza nchini, Mhe:Marianna Young nae ameendelea kuishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuonyesha ushirikiano mzuri kwa Uingereza katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo na kibiashara.

Aidha pia Balozi Young ameongeza kwa kuwa serikali ya Uingereza itaendelea kusimama kama mdau na mshirika wa maendeleo kwa Tanzania pamoja na kudumisha mahusiano ya kidiplomasia ambayo yameendelea kudumu kwa muda mrefu mpaka sasa.

Maadhimisho hayo ya siku ya mfalme yalifanyika Juni 10, 2025 katika makazi ya balozi wa Uingereza yalioko jijini Dar es salaam.