Momba, Songwe
Kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Kipanda lenye urefu wa mita 20 na upana mita 7 kumeleta ahueni kwa wakazi wa vijiji vya Namsinde na Mfuto kuzifikia kwa urahisi huduma za kijamii na kiutawala zinazopatikana Makao Makuu ya kata hiyo Myunga wilayani Momba mkoani Songwe.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Momba na Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Suleiman Mkopi amesema kuwa hapo awali wananchi walikuwa wakipata adha kubwa kutokana na mawasiliano kukatika hasa kipindi cha masika kati ya vijiji vya Namsinde, Mfuto na maeneo mengine ambapo ilikuwa ni shida kwao kufika Makao Makuu ya Kata hiyo Myunga.
“Kukamilika kwa daraja hili kumerahisisha shughuli za kiuchumi, vijiji vya Namsinde na Mfuto ni wakulima wakubwa wa mahindi na maharage, daraja hili limesaidia kusafirisha mazao yao kwa kipindi chote cha mwaka”, amesema Mhandisi Mkopi.
Ameeleza kuwa daraja hilo pia limerahisisha shughuli za kijamii na kiutawala ambapo upande wa Myunga ambayo ni Makao Makuu ya kata, ndipo zinapatikana huduma za kijamii hususani elimu na afya ambazo zinatolewa kupitia shule ya msingi Myunga pamoja na kituo cha afya Myunga.
Bw. Bernard Sadox mkazi wa kijiji cha Myunga ameishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja hilo kwani pamoja na kuwasaidia kusafirisha mazao yao kwa urahisi lakini pia daraja hilo limewasaidia kuzifikia huduma za afya kwa wakati na kwa urahisi.
Naye, Bi. Neema Kavundwa mkazi wa kijiji cha Lwasho amesema kuwa kukamilika kwa daraja hilo ni ukombozi hasa kwa akina mama wajawazito na wagonjwa wengine kutoka vijiji vya Namsinde na Mfuto ambao walikuwa wakipata changamoto ya kuvuka hasa kipindi cha masika ambapo mto ulikuwa ukijaa hivyo kuwa kikwazo kuzifikia huduma za afya.
“Kwakweli watu tulikuwa tunapata shida, mto ukijaa ilibidi tuvushwe kwa kubebwa lakini sasa tunavuka vizuri daraja limekamilika na tunasafirisha mazao yetu bila shida yoyote, tunaishukuru serikali”.
