Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ukiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lughano Kusiluka, leo Jumanne Septemba 09, 2025, umetembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya UDOM mkoani Njombe.
Katika ziara hiyo, Profesa Kusiluka ameonesha kuridhishwa na hatua zilizofikiwa, huku akimhimiza mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji ili mradi huo ukamilike kwa wakati kama ilivyopangwa.

“Tumeelekeza Mkandarasi kuongeza nguvu kazi na vifaa vya ujenzi, na kuhakikisha kazi inaendelea usiku na mchana. Hakutakuwa na nyongeza ya muda, hivyo matarajio yetu ni kuona majengo yamekamilika ifikapo Mei 2026,” amesisitiza
Ameahidi Menejimenti ya Chuo kuweka utaratibu wa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa maendeleo ya ujenzi, badala ya kuwategemea watalaamu na Mshauri pekee ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati uliopangwa na Wizara.
Kwa upande wake, Mshauri Elekezi wa Mradi, Mhandisi Filbert Shayo, amesema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 15, ambapo kwa sasa Mkandarasi kwa Majengo yote, yuko kwenye hatua za kukamilisha Ujenzi wa msingi na kuanza maandalizi ya hatua zinazofuata.
Ziara hiyo ililenga kutoa taswira halisi ya maendeleo ya ujenzi na kufanya tathmini ya mwenendo wa kazi, huku ikitoa mwelekeo wa kuhakikisha malengo ya muda na ubora wa mradi yanazingatiwa.

Akizungumza hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka, aliutaka uongozi wa UDOM kuhakikisha wanasimamia kwa karibu ujenzi wa majengo hayo, kwani Mkoa una matarajio makubwa kwamba mwaka ujao wa masomo 2026/27 wananchi wa Njombe na mikoa Jirani wataanza kudahiliwa kwenye chuo hicho.
Kupitia mradi huu, Chuo Kikuu cha Dodoma kinatarajia kuanzisha masomo ya Biashara, Kilimo, Sayansi na Teknolojia ili kuendana si tu na mahitaji ya soko, lakini mahitaji ya wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ambao wamekuwa wakijihusisha zaidi na Biashara itokanayo na mazao ya Misitu na Kilimo.


