Na Berensi China, JamhuriMedia, Meatu

Ujenzi wa daraja kubwa la Mto Itembe, linalounganisha Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu na Mkalama mkoani Singida, umefikia asilimia 85 na umeleta faraja kwa wananchi walioteseka kwa muda mrefu kutokana na changamoto za usafiri hasa wakati wa mvua.

Wananchi wa maeneo hayo wamesema wamekuwa wakikumbana na kero kubwa ya kutoweza kuvuka mto kwa siku kadhaa, hali iliyosababisha vifo vya watu, mifugo na uharibifu wa mali. Wameishukuru serikali na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kusimamia ujenzi huo, huku wakifurahishwa na ukweli kuwa kazi hiyo inatekelezwa na mkandarasi mzawa.

Mkandarasi anayejenga daraja hilo ni kampuni ya RockTronick, ambapo msimamizi wa mradi huo, Eng. Emanuel Kisanga, amesema ujenzi huo wenye urefu wa mita 150 ulisimama kwa miezi saba kutokana na ukosefu wa fedha, lakini hivi karibuni malipo yamepatikana na wanatarajia kumaliza kazi hiyo ifikapo Septemba mwaka huu.

Kwa upande wake, Mhandisi Raphael Chasama kutoka TANROADS Simiyu amesema mradi huo umegharimu Shilingi bilioni 8.4 na utakamilika kwa viwango vya juu. Aidha, daraja hilo litaunganisha mikoa ya Singida, Simiyu, Manyara, Arusha na Mwanza, hivyo kurahisisha usafiri na uchumi wa wananchi.

“Tunaipongeza serikali kwa kutoa fedha na kutuwezesha kutumia wakandarasi wazawa wenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi bora nchini,” alisema Chasama.