Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amesema kuwa ziara ya Rais wa Msumbiji Daniel Chapo ni ishara tosha kuwa Afrika inafuatilia kwa karibu maendeleo yanayopatikana katika sekta ya miundombinu barani humo.
Kadogosa alitoa kauli hiyo mara baada ya Rais Chapo kukagua treni ya kisasa ya reli ya mwendokasi (SGR) jijini Dar es Salaam .
Ameeleza kuwa ujio huo si tu wa heshima bali unaashiria mshikamano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji.
“Tanzania na Msumbiji zimekuwa na uhusiano wa kihistoria tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Ushirikiano wetu umekuwa wa karibu katika masuala ya kisiasa, kiulinzi, kijamii, na hata kiutamaduni,” alisema Kadogosa.
Aliongeza kuwa mahusiano ya watu wa mataifa haya mawili yamekuwa ya karibu, akitoa mfano wa jamii ya Wamakonde waliopo pande zote mbili, ambao wanashirikiana kwa karibu na kuwa na mila zinazofanana.
