UKRAINE kwa mara nyingine imefanya mashambulizi makubwa ya ndege zisizo na rubani kwenye mikoa ya Urusi

Mashambulizi hayo ya usiku kucha wa kuamkia siku ya Jumamosi yamesababisha milipuko katika miundombinu ya kuchakata mafuta.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema hii leo asubuhi kwamba zaidi ya ndege 100 zisizo na rubani za Ukraine zimedunguliwa.

Mamlaka katika mikoa iliyoathirika ya Samara, Penza na Ryazan zimethibitisha mashambulio hayo ya droni na zimesema kuwa mabaki ya ndege hizo zisizo na rubani yalidondoka kwenye maeneo ya viwanda, lakini hakuna uharibifu mkubwa uliotokea na pia hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Maafisa wa Ukraine wamesema mashambulizi yao ya ndege zisizo na rubani yanalenga kutatiza uwezo wa kijeshi wa Urusi kwa kuyashambulia maghala ya mafuta, risasi na miundombinu ya usafirishaji.