Ukraine inaendelea kulemewa vibaya na mashambulizi ya Urusi kwa takribani miaka minne sasa tangu uvamizi huo bila ya dalili ya vita hivyo kupata ufumbuzi licha ya hatua kadhaa zilizochukuliwa na washirika wa Kiev.
Alfajiri ya Jumanne (Januari 20), vikosi vya Urusi viliripotiwa kufanya mashambulizi yaliyojumuisha droni na makombora dhidi ya mji mkuu, Kiev, ambako moto mkubwa ulizuka na umeme kukatika.
Meya Vital Klitschko aliandika kupitia mtandao wa Telegram kwamba mashambulizi kwenye ukingo wa mashariki wa Mto Dnipo yalilipiga jengo lisilokaliwa na raia na kumjeruhi mtu mmoja.
“Vifaa kutokana na droni hiyo viliangukia kwenye eneo moja na mifumo ya umeme iliharibiwa,” aliandika meya huyo.
Mkuu wa utawala jeshi, Tymur Tkachenko, alithibitisha kuwa ghala moja liliharibiwa na magari kadhaa kuteketea kwa moto kutokana na mashambulizi hayo ya Urusi.



