Mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi inaripotiwa kuzidunguwa zaidi ya droni 100 za Ukraine usiku wa kuamkia leo kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, zikiwemo zile zilizoelekezwa kwenye mji mkuu, Moscow.

Kwa mujibu wa maafisa wa Urusi, mashambulizi hayo ni sawa na yale yaliyofanyika wiki iliyopita, ambapo pia Moscow na miji mingine ililengwa.

Meya wa mji wa Moscow, Sergei Sobyanin, amesema kupitia mtandao wa Telegram kwamba vikosi vya wizara ya ulinzi vilizidunguwa droni 27 zilizokuwa zikielekea mji mkuu huo wa Urusi.

Mapema, wizara hiyo ya ulinzi ilisema vikosi vyake vilizidunguwa droni 112 baina ya saa tatu na saa sita usiku wa kuamkia leo.

Urusi pia ilituma mkururo wa droni kuelekea Ukraine wiki iliyopita, ambapo Rais Volodymyr Zelensky alisema ndani ya siku tatu tu, Moscow ilisharusha zaidi ya droni 900 kuelekea Kiev.