Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Antonio Costa, amesema shambulio lolote dhidi ya miundombinu ya kiraia kama ile ya nishati sio halali na haikubaliki hata kidogo.
Hii ni baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutoa muda wa hadi kesho Jumanne kwa Iran kuufungua Mlango Bahari wa Hormuz au miundo yake ishambuliwe vibaya.
Iran iliufunga mlango huo muhimu unaopitisha asilimia 20 ya mafuta ya dunia, kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Antonio Costa amesema kuongezeka kwa mashambulizi hakutaleta faida yoyote katika vita hivyo huku akisisitiza kuwa majadiliano pekee ndio yanayoweza kuleta suluhu ya mgogoro uliopo.
Kauli yake inajiri wakati kukiwa na ripoti za Marekani na Iran kupokea rasimu ya pendekezo la usitishwaji vita kwa siku 45.
Pendekezo hilo linalodaiwa kuwasilishwa na wapatanishi kutoka Misri, Pakistan na Uturuki kwa mataifa hayo hasimu, lilitumwa usiku wa jana kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, pamoja na mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, Steve Witkoff.



