Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, ametoa siku 28 kwa Wizara ya Ujenzi pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Kagera kuhakikisha wanakamilisha taratibu za kusitisha mkataba na kumfukuza kazi mkandarasi aliyeshindwa kutekeleza ujenzi wa barabara ya kilomita 50 ya Kyerwa–Omurushaka kwa kiwango cha lami.
Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa serikali, TANROADS, mkandarasi pamoja na wananchi wa eneo hilo, Waziri Ulega amesema barabara hiyo ilikuwa nyenzo muhimu ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Kyerwa, lakini imeshindwa kuleta tija kutokana na uzembe wa mkandarasi.
“Serikali haiwezi kuendelea kuvumilia wakandarasi wanaochelewesha miradi ya kimkakati. Ndani ya siku 28 nataka mchakato wa kusitisha mkataba ukamilike,” alisema Waziri Ulega.
Aidha, Waziri huyo ameiagiza TANROADS Makao Makuu kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matumizi ya shilingi bilioni 9.15 zilizolipwa kwa mkandarasi kama malipo ya awali, akisisitiza kuwa mtumishi yeyote atakayebainika kuhusika na ubadhirifu wa fedha hizo atachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa kwenye kesi ya uhujumu uchumi sambamba na mkandarasi.
Pia ameiagiza wizara hiyo kuhakikisha mkandarasi mzawa anapatikana haraka ili kuendelea na kazi ya ujenzi wa barabara hiyo, lengo likiwa ni kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na wananchi waanze kunufaika.
Hatua hiyo inakuja baada ya mkandarasi Shandong Luqiao Co. Ltd, aliyepewa zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo yenye thamani ya shilingi bilioni 94.3, kushindwa kufikia hata asilimia 50 ya utekelezaji wa mradi, ambapo hadi sasa amefikia asilimia 5.4 pekee, licha ya kupokea bilioni 9.15 kama malipo ya awali.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Joel Samwel Mwambungu, amesema mkandarasi huyo amekuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa mradi kutokana na uhaba wa vifaa na wafanyakazi, hali iliyoathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, huku muda wa utekelezaji wa mradi ukiwa tayari umetumika kwa asilimia 43.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajat Fatma Mwassa, amesema kutokana na utendaji duni wa mkandarasi huyo, hapasi kuendelea kupewa zabuni nyingine ndani ya mkoa wa Kagera, na baadhi ya miradi aliyokabidhiwa inapaswa kunyang’anywa.
“Wamepokea fedha nyingi kwa muda mrefu lakini hakuna kazi ya kuridhisha iliyofanyika. Wananchi wanateseka, barabara ni mbovu, nauli zinaongezeka, wakati hata nchini kwao hawana barabara mbovu hata moja. Serikali inapaswa kuwachukulia hatua mara moja kwa maslahi ya wananchi wetu,” alisema RC Mwassa.
Wananchi
Wananchi wa Kyerwa wamesema kuchelewa kukamilika kwa barabara hiyo kumeathiri kwa kiwango kikubwa maisha yao, hasa katika usafirishaji wa mazao, biashara na huduma za kijamii. Wamesema barabara mbovu imesababisha gharama za usafiri kupanda, magari kushindwa kufika vijijini na wakulima kushindwa kufikisha mazao yao sokoni kwa wakati, hali inayowaongezea umaskini.
Wananchi hao wameiomba serikali kuhakikisha maagizo ya Waziri Ulega yanasimamiwa kikamilifu ili mkandarasi aondolewe na kazi ya ujenzi ianze upya haraka kwa lengo la kuondoa mateso waliyo nayo kwa muda mrefu.








