Mamilioni ya watu wanaokimbia vita nchini Sudan wanakabiliwa na kitisho kikubwa zaidi cha njaa, wakati wakisaka hifadhi kwenye nchi ambazo tayari zina uhaba wa chakula.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP lilisema siku ya Jumatatu kwamba wakimbizi zaidi ya milioni 4 huenda wakawa hatarini zaidi na hasa kwa kuwa misaada itapungua huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Misri, Ethiopia, Libya, Uganda na Chad.

Mratibu wa Dharura wa WFP Shaun Hughes amesema ingawa wakimbizi kutoka Sudan wanakimbia ili kuokoa maisha yao lakini bado wanakabiliwa na njaa, kukata tamaa, na rasilimali chache huko wanakokimbilia.

Ukosefu wa chakula na njaa imeenea kote Sudan, taifa linalokabiliwa na vita baina ya jeshi la kitaifa na wanamgambo wa RSF.

Karibu watu 40,000 wameuawa na karibu milioni 13 wameyakimbia makazi yao.