Kaimu Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa mgogoro katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa Kongo, unazidi kuongezeka.

Vivian van de Perre amesema licha ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kuondoka mwezi Januari katika mji wa Uvira kufuatia shinikizo la kimataifa, mapigano yanazidi kuongezeka katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini kati ya kundi hilo na jeshi la Kongo, na kwamba matumizi ya silaha nzito na droni yanahatarisha kwa kiasi kikubwa maisha ya raia.

Mjumbe huyo ameendelea kutahadharisha kuwa hali huko Kivu Kusini bado ni tete na kwamba kumezuka uhasama mpya unaotanua mzozo huo katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na mkoa wa Tshopo na eneo la mpakani mwa Burundi, jambo linalozidisha hatari ya kuzuka kwa vita vya kikanda.