Umoja wa Mataifa umeitaka Iran kusitisha mpango wa kutekeleza hukumu ya kifo kwa waandamanaji waliokamatwa na ichunguze taarifa zote za vifo kwa uhuru na uwazi.

Wito huo umetolewa jana na Martha Pobee, katibu mkuu msaidizi wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya siasa na kudumisha amani, alipokuwa akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amezitaka pande zote kujizuia huku akiamini kuwa masuala yote yanayohusu Iran yanaweza kutatuliwa vyema kupitia diplomasia na mazungumzo.

Mamlaka za Iran zinatuhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi zinapojaribu kuyazima maandamano ambayo tayari yamesababisha vifo vya maelfu ya watu. Marekani imeonya kuwa ipo tayari kutumia njia zote ili kukomesha ukandamizaji huo.