Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Urambo
HALMASHAURI ya Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora imefungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali, kwa kuanzia wametenga eneo la ardhi lenye ukubwa wa hekari 72 kwa ajili ya kazi hiyo.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Grace Quintine alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya halmashauri katika kikao cha baraza la madiwani.
Amesema kuwa halmashauri hiyo ni miongoni mwa halmashauri zenye mazingira bora ya uwekezaji na ardhi nzuri inayofaa kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara.

Amedokeza kuwa maboresho makubwa ya miundombinu ya huduma za kijamii ambayo yameendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni kivutio muhimu kwa wawekezaji.
Guintine amefafanua kuwa Urambo ni mahali salama kwa uwekezaji na kwa mwaka huu wa fedha wameratibu maeneo maalumu yanayofaa kwa uwekezaji na kutenga eneo lenye ukubwa wa hekari 72 katika Kata za Usoke na Kapilula.
Aliongeza kuwa mbali na uwekezaji huo, halmashauri pia imeendelea kuandaa mazingira yatakayosaidia kufanikisha utekelezaji shughuli za maendeleo ikiwemo kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kufanikisha utekelezaji shughuli zake.

‘Kwa sasa tunafuatilia upatikanaji wa zaidi ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ukamilishaji baadhi ya miradi na kuratibu upatikanaji wa maeneo mengine ya uwekezaji katika Wilaya hiyo,’ ameeleza.
Mkurugenzi amefafanua kuwa mwaka jana halmashauri hiyo iliidhinishiwa na bunge mapato na matumizi ya kiasi cha shilingi bil 39.3 ila hadi kufikia Novemba 30, 2025 walikuwa wamekusanya jumla ya shilingi bil 15 kutoka vyanzo vya ndani.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Athumani Mwiniko ameeleza kuwa madiwani watashirikiana ipasavyo na watalaamu ili kuhakikisha shughuli za maendeleo zinatekelezwa ikiwemo kuongeza vyanzo vipya ya mapato.
Ametoa wito kwa madiwani, wataalamu na watendaji wa vijiji na kata kushirikiana ipasavyo na kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.


