Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilitaja tukio hilo kuwa “shambulio la kigaidi,” huku ikisema Rais Vladimir Putin amearifiwa.

Mamlaka zilizowekwa na Urusi katika eneo la Kherson nchini Ukraine zimesema zaidi ya watu 24 wameuawa baada ya shambulio la droni la Ukraine kupiga sherehe za mkesha wa Mwaka Mpya katika kijiji cha Khorly, kilichopo pwani ya Bahari Nyeusi.

Kiongozi wa utawala unaoungwa mkono na Urusi mkoani Kherson, Vladimir Saldo, alisema droni tatu zilipiga mgahawa uliokuwa umejaa watu, na kusababisha vifo zaidi ya 24 pamoja na majeruhi wasiopungua 25. Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilitaja tukio hilo kuwa “shambulio la kigaidi,” huku ikisema Rais Vladimir Putin amearifiwa.

Hata hivyo, jeshi la Ukraine limekanusha madai hayo, likiyataja kama upotoshaji wa taarifa na kusisitiza kuwa linashambulia malengo ya kijeshi pekee kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky hakutoa kauli ya moja kwa moja kuhusu tukio hilo.

Wakati huo huo, Urusi na Ukraine zimeripoti mashambulizi makubwa ya droni pande zote mbili, katika ishara ya kuendelea kwa mapigano makali karibu miaka minne tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi kamili dhidi ya Ukraine.