Urusi imesema imekiteka kijiji kingine magharibi mwa mkoa wa Donesk nchini Ukraine Jumapili 13.07.2025 wakati vikosi vyake vikiendelea kupata mafanikio na kusonga mbele kuelekea katika mkoa jirani wa Dnipropetrovs.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imekitaja kijiji hicho kuwa ni cha Myrne kilicho karibu na mpaka kati ya mikoa hiyo. Wakati Moscow ikitangaza mafanikio hayo, Shirika la Ujasusi la Ukraine limearifu kuwa limewauwa watu wawili wanaoshukiwa kuwa walimuuwa jasusi wa Ukraine mjini Kyiv Alhamisi wiki hii.
Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Ukraine Vasyl Malyuk, amesema watu hao, mwanamke na mwanaume waliokuwa mafichoni wakati wa operesheni maalumu waligoma kujisalimisha na walianzisha mapambano ya risasi ambapo hatimaye waliuawa.
