Ikulu ya Urusi imepuuzilia mbali mazungumzo kuhusu mkutano kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na Volodymyr Zelensky wa Ukraine, huku Donald Trump akitoa wito kwa viongozi hao wawili kukutana ili kujadili kumaliza vita nchini Ukraine.

Shinikizo la kufanyika kwa mkutano baina ya nchi hizo mbili linakuja baada ya rais wa Marekani kukutana na Putin mjini Alaska wiki iliyopita, na kuwakaribisha viongozi saba wa Ulaya na Zelensky katika Ikulu ya White House siku ya Jumatatu.

Trump alikiri mzozo huo ulikuwa “vigumu” kusuluhisha na akakubali kuwa inawezekana rais wa Urusi hakutaka kumaliza uhasama.

“Tutajua kuhusu Rais Putin katika wiki kadhaa zijazo,” alisema Jumanne. “Inawezekana kwamba hataki kufanya makubaliano.”

Putin alikabiliwa na “wakati mgumu” ikiwa ndivyo ilivyokuwa, Trump aliongeza, bila kutoa maelezo yoyote.

Rais wa Urusi siku ya Jumatatu alimwambia Trump kuwa yuko “sawa” na wazo la mazungumzo ya moja kwa moja na Ukraine, lakini siku iliyofuata Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov alipuuzilia mbali ahadi hiyo hatua ambayo tayari haijaeleweka.

Mkutano wowote ungepaswa kutayarishwa “hatua kwa hatua… kuanzia ngazi ya wataalam na baada ya hapo kupitia hatua zote zinazohitajika”, alisema, akirudia maneno ya mara kwa mara ya Urusi.

Dmitry Polyanskiy, naibu mwakilishi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, aliiambia BBC “hakuna mtu [aliyekataa]” fursa ya mazungumzo ya moja kwa moja, “lakini haipaswi kuwa mkutano kwa ajili tu ya mkutano uwe umefanyika”.

Siku ya Jumanne, iliripotiwa kwamba Putin alikuwa amependekeza kwa Trump kwamba Zelensky anaweza kusafiri hadi Moscow kwa mazungumzo, jambo ambalo Ukraine haikuweza kukubali kamwe.

Pendekezo hilo linaweza kuwa ni njia ya Urusi ya kuweka chaguo lisilowezekana ambalo Ukraine haiwezi kukubaliana nalo.