Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda, amesema mfuko huo umeingia mikataba ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 1,974 zenye vijiji 5,111 na wakazi wapatao 29,154,440. Kupitia mikataba hiyo, jumla ya minara 2,152 inatarajiwa kujengwa kwa lengo la kuboresha sekta ya mawasiliano nchini.

Akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) jijini Dar es Salaam jana, Mhandisi Mwasalyanda alisema hadi sasa miradi iliyokamilika inahusisha kata 1,661, vijiji 4,570 na wakazi 25,148,031, ambapo minara 1,810 tayari imekamilika.

“Mei 2023, serikali kupitia UCSAF iliingia mikataba na watoa huduma kufikisha mawasiliano vijijini kupitia mradi huu. Kata 713 zitafaidika, minara 758 itajengwa, na wilaya 127 kutoka mikoa 26 zitahusishwa. Wananchi wapatao milioni 8.5 watanufaika kwa kutumia ruzuku ya Sh bilioni 126,” alisema Mhandisi Mwasalyanda.

Aliongeza kuwa minara 304 iliyokuwa ya teknolojia ya 2G imeboreshwa hadi kufikia 3G/4G, ambapo ruzuku ya Sh bilioni 5.51 ilitumika na kazi hiyo imekamilika kwa asilimia 100.

Kwa mujibu wa taarifa ya Machi 2025 kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), idadi ya laini za simu nchini imeongezeka kutoka milioni 54 mwaka 2021 hadi milioni 90.4 Machi mwaka huu. Vilevile, watumiaji wa intaneti wameongezeka hadi milioni 49.3 ikilinganishwa na milioni 29.8 mwaka 2021.

“Uwekezaji huu hauishii kwenye ujenzi wa miundombinu pekee, bali pia tunatoa mafunzo kwa walimu wa shule za sekondari ili kuwawezesha kuwasaidia wanafunzi wao kuendana na kasi ya mabadiliko ya TEHAMA,” aliongeza Mwasalyanda.

Kuhusu visiwani Zanzibar, Mhandisi Mwasalyanda alisema UCSAF ilisaini mkataba Januari 2022 kwa kushirikiana na kampuni ya Zantel/Honora. Kupitia mradi huo, Shehia 38 zimenufaika na minara 42 imejengwa kwa kutumia ruzuku ya Sh bilioni 6.9.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Bakari Kimwanga, alisema kikao hicho kimewapa uelewa mpana kuhusu UCSAF na kuwasihi wahariri wasisite kushirikiana na mfuko huo pindi wanapohitajika.

Aidha, alisisitiza kuwa jitihada zaidi zinahitajika ili kuhakikisha maeneo yote yasiyo na mawasiliano nchini yanafikiwa ipasavyo.