RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Zanzibar imeimarika kutokana na utekelezaji wa malengo ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kuwaunganisha wananchi, kuleta ustawi wao na kukuza uchumi.
Dk Mwinyi alisema hayo jana katika hotuba yake kwa Baraza la Wawakilishi akieleza mafanikio ya kipindi cha miaka mitano tangu aingie madarakani.
Alisema utekelezaji wa malengo hayo umesababisha Uchumi wa Zanzibar kukua kwa asilimia 7.1 mwaka 2024 huku pato la taifa likiongezeka hadi kufika thamani ya Sh trilioni 6.57 mwaka 2024 kutoka Sh trilioni 4.78 mwaka 2021.
Alibainisha ukuaji huo ni sawa na ongezeko la asilimia 63 ambapo pato la wananchi limeongezeka kufika Sh milioni 3.22 mwaka 2024 kutoka Sh milioni 2.52 mwaka 2020.
Aidha, Rais Dk Mwinyi alieleza utekelezaji wa malengo ya serikali umesababisha pia ukusanyaji wa mapato ya serikali kuongezeka kutoka Sh bilioni 856 mwaka 2020/2021 hadi Sh trilioni 2.104 mwaka 2023/2024.
Kadhalika, Dk Mwinyi alisema ongezeko hilo katika eneo la ukusanyaji wa mapato ni sawa na ongezeko la Sh trilioni 1.248.
Aliongeza hali ya mfumuko wa bei umekuwa wa kupanda na kushuka kutokana na kuongezeka kwa huduma na bidhaa katika soko la dunia na kwamba kwa Zanzibar mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 5 mwaka 2024.
“Tumeweza kudhibiti hali ya mfumuko wa bei na kuuwezesha kubaki katika tarakimu moja,” alithibitisha Rais Dk Mwinyi huku akijivunia mafanikio hayo.
Alieleza ili kuwa na utekelezaji mzuri wa malengo ya serikali, bajeti ya serikali imeongezeka hadi kufika Sh trilioni 5.1 mwaka 2024/2025 kutoka Sh trilioni 1.579 mwaka 2020/2021 ambao ni sawa na ukuaji wa asilimia 228.
Kwa upande mwingine, Rais Mwinyi alisema bajeti ya maendeleo imeongezeka kutoka Sh bilioni 609.9 mwaka 2020/2021 hadi Sh trilioni 3.271mwaka 2024/2025 sawana ongezeko la asilimia 436.33.
Alisema kwa lengo la kuhakikisha serikali inakuwa na fedha muda wote za kutekeleza malengo ya maendeleo, serikali imeanzisha Mpango wa Hati Fungani (SUKUK) inayofuata misingi ya sharia.
“Katika awamu ya kwanza ya mpango huu, serikali imeweza kukusanya asilimia 128 ya lengo la makusanyo ya shilingi bilioni 300,” alisema.
Aliongeza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika jitihada za serikali za kuvutia wawekezaji ambapo kasi ya uwekezaji imeongezeka na kwamba hadi kufika Juni 2025, miradi 485 ya Dola za Marekani bilioni 6.2 imesajiliwa na Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).
Alisema miradi hiyo kwa hakika inatarajiwa kuongeza ajira 25,470. Miradi hiyo inahusisha sekta za hoteli zenye miradi 187, biashara ya majengo miradi 112, viwanda miradi 48, kilimo miradi 27, michezo miradi 28 na sekta zingine miradi 83.
Alitanabaisha kuwa kwa lengo la kurahisisha na kukuza utalii, serikali iliruhusu uwekezaji kwenye visiwa vidogo ambapo hadi sasa Zipa imesajili miradi katika visiwa 17 inayotarajiwa kuwekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 377.5.
Uwezeshaji wananchi kiuchumi
Rais Mwinyi alisema serikali imefanikiwa kupambana na umasikini kwa kuwawezesha wananchi kiuchumi ambapo hadi Mei 2025 mikopo 5,366 ya Sh bilioni 39.4 ilitolewa na Wakala ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa wananchi 25,701 wakiwemo wananchi 1,560 wa makundi maalumu.
Sekta ya viwanda yakua
Alieleza kuwa mafanikio pia yalipatikana katika jitihada za kuvutia sekta ya viwanda kwa kuboresha barabara na huduma za kijamii kama maji na afya huku serikali ikiendelea kuvutia uwekezaji katika eneo hilo na nyaraka za ukodishaji wa ardhi zikitolewa kwa wawekezaji 12.
Dk Mwinyi alisema serikali yake imetangaza vitalu 10 vya mafuta na gesi kwa wawekezaji kwa ajili ya utafutaji wa maafuta na gesi.
Uzalishaji wa samaki wapaa
Alisema serikali imeimarisha miundombinu ya uvuvi kwa kukamilisha ujenzi wa soko la Samaki la Kisasala Malindi ambalo limeanza kuhudumia wastani wa watu 10,000.
“Jitihada za serikali zimechochea kuongezeka kwa uzalishaji wa samaki wanaovuliwa kwa asilimia 107.2 kutoka tani 38,107 mwaka 2020 zenye thamani ya Shilingi bilioni 205.35 hadi kufika tani 78,943 mwaka 2024 zenye thamani ya Shilingi bilioni 618.18,” alisema.
Rais Dk Mwinyi alifahamisha kuwa jitihada za kuimarisha upatikanaji wa huduma za umeme zimepata mafanikio kwa kuongezeka idadi ya wananchi walioungiwa umeme hadi kufika 138,065 baada ya serikali kupunguza gharama za kuweka umeme.
Aidha, Rais Dk Mwinyi alisema ili kutoa nafasi ya matayarisho kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, amelivunja rasmi Baraza la Wawakilishi kuanzia Agosti 13, 2025 kwa madaraka aliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 91 (2) (a) cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.
