*Rais Samia aonesha utashi mkubwa kuendeleza sekta ya madini
*Ujenzi wa maabara za kisasa kuleta mapinduzi ya huduma Barani Afrika
- Mchakato wa ununuzi wa helikopta waendelea kwa kasi
*Wataalamu wa GST kujengewa uwezo
*Kamati yashauri GST kujengewa uwezo zaidi
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuonesha dhamira na utashi mkubwa wa kuendeleza Sekta ya Madini kupitia uwekezaji mkubwa katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), hatua inayolenga kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya taifa.
Hayo yamebainishwa leo Januari 19, 2026 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, alipokuwa akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ambapo amesema kuwa mazingira ya kisiasa na kiuongozi yaliyopo kwa sasa ni muafaka wa kuchukua hatua za kimkakati za kukuza sekta ya madini kwa manufaa ya taifa.
Amesema dhamira thabiti ya Rais Samia imeiwezesha Wizara ya Madini kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo kuimarisha tafiti za jiolojia ambazo ni nguzo kuu ya ukuaji wa Sekta ya Madini na kichocheo cha uwekezaji.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali kupitia GST ipo katika hatua za mwisho za ununuzi wa helikopta maalum kwa ajili ya tafiti za jiolojia, hatua itakayosaidia kuongeza kiwango cha utafiti kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia angalau asilimia 50. Tafiti hizo zitakuwa na mwelekeo maalum wa kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapatia taarifa sahihi za maeneo yenye rasilimali za madini.
Waziri Mavunde amesema mpaka sasa Serikali kupitia GST imefanikiwa kutekeleza tafiti mbalimbali za msingi ikiwemo Utafiti wa High Resolution Airborne Geological Survey kwa asilimia 16, Geological Mapping kwa asilimia 97, Geochemical Survey kwa asilimia 24 pamoja na Low Resolution Airborne Geological Survey kwa asilimia 100.
Ameeleza kuwa GST ni chanzo kikuu cha taarifa za awali zilizoibua migodi mikubwa mingi nchini, jambo linaloonesha umuhimu wa taasisi hiyo katika kuvutia wawekezaji na kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya madini.
Ameongeza kuwa Sekta ya Madini imefungamanishwa kwa karibu na sekta nyingine muhimu ikiwemo kilimo, maji, afya na viwanda, ambapo tafiti za jiolojia husaidia kubaini maeneo yenye udongo wenye rutuba, upatikanaji wa maji pamoja na rasilimali nyingine muhimu kwa maendeleo endelevu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amesema Tanzania bado inaagiza mbolea kutoka nje kwa kiwango kikubwa, lakini kukamilika kwa tafiti za madini kutatoa fursa ya kuanzishwa kwa viwanda vya mbolea hapa nchini, hivyo kupunguza gharama na kuimarisha uzalishaji wa kilimo.
Amesisitiza kuwa GST ina jukumu la kufanya tafiti za jiolojia, uchunguzi wa sampuli za miamba na madini, utambuzi wa aina na kiasi cha madini, vipimo vya jioteknolojia pamoja na tafiti za uchenjuaji wa madini kwa ajili ya matumizi ya ujenzi na uchimbaji.
Waziri Mavunde amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za ujenzi wa maabara kubwa na za kisasa (State of the Art Laboratories) zitakazohudumia wataalamu wa ndani na nje ya nchi, zikiwemo maabara za Dodoma – Kizota, Geita na Chunya, ambapo ujenzi wake unaendelea.
“Ujenzi wa maabara hizi utaifanya Tanzania kuwa kituo muhimu cha huduma za maabara za madini Barani Afrika,” amesema Mavunde.
Ameongeza kuwa Serikali imefikia makubaliano na wataalamu kutoka Finland pamoja na Taasisi ya KIGAM kwa ajili ya kujenga uwezo wa watumishi wa GST ili kuhakikisha taasisi hiyo inakuwa na wataalamu wa kutosha na wenye ujuzi wa kimataifa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Steven Kiruswa, ameipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa maswali na ushauri wake, akisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia ni nguzo muhimu katika shughuli za madini. Amesema GST ndiyo kitovu cha taarifa za miamba, madini na udongo nchini.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Simon Songe, ameipongeza Wizara ya Madini kwa juhudi zake za kuiwezesha Kamati kupata uelewa mpana wa masuala ya sekta ya madini na taasisi zake, huku akishauri GST kuendelea kujengewa uwezo zaidi ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sekta.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhamasishaji, Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), Marium Mgaya, amesema taasisi hiyo ina jukumu la kuhakikisha mapato yatokanayo na rasilimali hizo yanahakikiwa, yanawekwa wazi na kunufaisha wananchi kwa mujibu wa Sheria ya TEITA ya mwaka 2015.
Ameongeza kuwa Sekta ya Uziduaji imeendelea kuimarika kutokana na usimamizi thabiti wa Serikali, na kuahidi kuendelea kushirikiana na Kamati ya Bunge ili kuhakikisha Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia inaendelea kukua na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
.






