Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
WANAWAKE waliofanya vizuri kwenye mchakato wa kura za maoni za udiwani na ubunge wa viti maalumu kupitia Umoja wa Wanawake (UWT) wametakiwa kuwa watulivu kwa kuwa uteuzi wa mwisho utafanywa na vikao vya ngazi za juu.
Wito huo umetolewa jana na Katibu wa Jumuiya hiyo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora Rhoda John Madaha alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake.

Amesema kuwa hii ni hatua ya awali ya mchakato wa kupata madiwani na wabunge wa viti maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mkoa huu na Mikoa mingine pia, mchakato huu bado unaendelea, washindi wote kuweni watulivu.
Rhoda amefafanua kuwa mkutano mkuu wa uchaguzi kwa watia nia wa ubunge kupitia UWT Mkoa umefanyika juzi katika ukumbi wa shule ya sekondari New Era mjini hapa ambapo jumla ya wagombea 8 walijitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa.
Wagombea hao ni Zena Mohamed (Shilole), Dk Bayoun Awadhi Kigwangala, Aziza Slyeum Ally, Jaqueline Kainja, Mkuame Abdul Isale (Mamy Baby), Zahara Muhidin Michuzi, Christina Solomon Mndeme na Rebeca Joseph Kashindye.
Katika uchaguzi huo Aziza Sleyum Ally alishika nafasi ya kwanza kwa kupata kura 1,133, Christina Mndeme nafasi ya pili (kura 1,011), Jaqueline Kainja nafasi ya tatu (kura 508) na Dk Bayoum Kigwangala nafasi ya nne (kura 269) .

Wengine ni Zena Mohamed Yusuph (Shilole) nafasi ya tano (kura 104), Mkuame Abdul Isale (Mamy Baby) nafasi ya sita (kura 84), Zahara Muhidin Michuzi nafasi ya saba (kura 30) na Rebecca Joseph Kashindye nafasi ya nane (kura 17).
Katibu ameeleza kuwa watia nia wote kwenye nafasi ya ubunge na udiwani wana nafasi sawa ya kuteuliwa kadri Chama kitakavyoona, na idadi ya watakaoteuliwa itategemeana na idadi ya wabunge wa majimbo na madiwani watakaochaguliwa.
Rhoda amebainisha kuwa jumla ya kura zilizopigwa na wajumbe wa mkutano wa UWT Mkoa ni 1,600, kura zilizoharibika zilikuwa nne (4) na jumla ya kura zote halali ni 1,596.

