Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Katika kuendeleza juhudi za kuhakikisha kila Mtanzania anatimiza haki yake ya kidemokrasia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, amejiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura katika kituo cha Chamwino Ikulu, mkoani Dodoma.

Rais Samia ametimiza zoezi hilo la uboreshaji wa taarifa zake leo Mei 17, 2025, ikiwa ni sehemu ya awamu ya pili ya uboreshaji wa daftari hilo linalosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Amefika kituoni majira ya saa 8:20 mchana na kuhitimisha zoezi hilo ndani ya dakika 10 tu ambapo pia ametumia nafasi hiyo kuzungumza na wananchi waliokusanyika kushuhudia tukio hilo kwa kuwaeleza umuhimu wa kujiandikisha na kuwa na nafasi ya kupiga kura.

Rais Samia ameeleza kuwa amejiandikisha rasmi Chamwino kutokana na nafasi yake ya sasa ya kuishi na kufanya kazi Dodoma, tofauti na miaka ya nyuma alipokuwa akijiandikisha Zanzibar.

“Mwaka huu nimeona ni vyema nifanye mabadiliko ya taarifa zangu hapa Chamwino, Makao Makuu ya nchi, ili niweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi nikiwa mkazi wa eneo hili,” amefafanua.

Amewahimiza wananchi wote kujitokeza kujiandikisha na kutumia haki yao ya kikatiba ya kushiriki katika chaguzi zijazo, akieleza kuwa kutoshiriki ni sawa na kujinyima fursa ya kuamua hatma ya taifa.

“Tusikose nafasi hii,huu ni mzunguko wa pili wa uboreshaji, na hatuwezi kurudi nyuma,ni wajibu wa kila Mtanzania kujiandikisha na hatimaye kushiriki uchaguzi,” amesema kwa kusisitiza.

Mbali na hayo amewataka maafisa wa uchaguzi kuwa wavumilivu na wanyenyekevu kwa wananchi, akiahidi kuwa serikali imejipanga kuhakikisha kila mwenye sifa ataandikishwa licha ya changamoto kama vile upungufu wa vitendea kazi.

Kwa upande wake, Afisa Mwandikishaji wa majimbo ya Chamwino na Mvumi, Godfrey Mnyamale, amebainisha kuwa idadi ya wanaojitokeza ni kubwa, huku lengo likiwa ni kuwaandikisha zaidi ya watu 280,000.

Amesema, “tunaendelea na zoezi hili kwa wale ambao walikosa awamu ya kwanza, wanaotaka kusahihisha taarifa au wale waliokuwa hawajatimiza vigezo wakati huo,hii ni nafasi nzuri kwao kutimiza wajibu wao,” amesema