Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam.

Afisa Mtendaji wa Dawasa Mkama Bwire ameeleza kuwa upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani unategemea sana vyanzo vya mvua.

Mkama ameeleza hayo alipokuwa akizungumza na wahariri na waandishi wa habari leo Desemba 12, 2025 kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika jiji la Dar es Salaam.

Mkama ameeleza kuwa pale mvua inapochelewa au kutonyesha kwa kiwango cha kutosha, uzalishaji wa maji hupungua kwa kiasi kikubwa.

“Vyanzo muhimu vya maji, kama mito, maziwa na visima, hulazimika kutegemea misimu ya mvua ili kujazwa tena na endapo mvua haitoshi uzalishaji wa maji unaweza kuyumba na kuathiri maelfu ya watumiaji,”anasema.

Alisema kuwa chanzo kikuu cha maji cha Mto Ruvu ndicho kinachohudumia sehemu kubwa ya Dar es Salaam.

“Kwa kawaida mtambo wa Ruvu Chini hudumia maeneo ya Bagamoyo, Kinondoni, Mwananyamala na Kariakoo ilhali Ruvu Juu husambaza maji maeneo ya Kibamba, Mbezi, Kinyerezi, Ubungo na Temeke.

“Hata hivyo kwa sasa uzalishaji wetu umeshuka kwa kiasi kikubwa hadi chini ya nusu ya uwezo wa kawaida kutoka zaidi ya lita milioni 270 kwa siku hadi lita milioni 50 kwa siku huku Ruvu Chini ukiwa mtambo uliyoathirika zaidi.

Mkama ameeleza kuwa kwa msimu huu walitarajia mvua za vuli kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba ambazo zingesaidia kuongeza kiwango cha maji katika Mto Ruvu lakini hali imekuwa tofauti mto umebadili mkondo wake kwa sehemu, kiwango cha joto kimeongezeka, na shughuli za kilimo na ufugaji ndani ya bonde zimeathiri upatikanaji wa maji.

“Watu wengi wanaoishi ndani ya bonde hili wamekuwa wakilitegemea kwa maisha yao tangu awali, jambo linalofanya kuwa vigumu kuwatenganisha na shughuli zinazochangia mabadiliko hayo,”anasema.

Aidha ameeleza hatua zilizochukuliwa ili kukabiliana na changamoto hiyo ni pamoja na kuongeza uzalishaji kupitia visima

“DAWASA imeanza kufufua na kukarabati visima vilivyokuwepo pamoja na kufunga pampu mpya ili kuongeza uzalishaji hatua hii inalenga kupunguza presha kwa mitambo ya Ruvu hasa kipindi hiki cha upungufu wa maji”amesema.

“Baadhi ya vibali vya matumizi mengine ya maji vimesitishwa ili kuhakikisha maji yaliyopo yanatosheleza matumizi ya wananchi,”amesema.

Aidha maji yaliyokuwa yakitegemewa kutoka Ruvu Chini sasa yanagawiwa pia kwa kutumia mtambo wa Ruvu Juu ili kufikia maeneo yaliyoathirika zaidi.

Mkama ameongeza kuwa wameanza kuhamasisha utamaduni wa kuhifadhi maji “Wananchi wanahimizwa kutumia matenki ili kuhifadhi maji nyakati ambayo yapo kwa sababu mara nyingi maji mengi yanayotokana na mvua huishia baharini na hayatarejea wakati wa kiangazi,”anasema

Katika hatua nyingine Mkama ameeleza kuwa serikali imeanza kutekeleza mikakati ya miradi ya muda mrefu kama bwawa la Kidunda.

“Ili kuhakikisha upatikanaji wa maji wa kudumu ujenzi wa Bwawa la Kidunda unaendelea na umefikia takribani asilimia 35 na tunatarajia kufikia mwishoni mwa mwaka 2026 bwawa liwe limekamilika,”anasema

Aidha bwawa hili litahakikisha upatikanaji wa maji wakati wote bila kutegemea mvua pekee.

Zaidi ya hapo bwawa hili litazalisha pia umeme na iwapo kutakuwa na maji ya kutosha yanaweza kutumika kwa shughuli zingine za kiuchumi.

Serikali imeanza utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji ambayo itasaidia maeneo tofauti kuweza kupata maji. Lengo ni kuhakikisha kuwa endapo chanzo kimoja kikiyumba, chanzo kingine kinaweza kusaidia bila kuathiri wananchi.

Aidha serikali imeanza uchimbaji wa visima vipya vya uzalishaji wa maji katika maeneo ya pembezoni mwa Dar es Salaam kama njia ya kuongeza vyanzo mbadala.