Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Profesa Sifuni Mchome amesema VETA itaendelea kuhakikisha Watanzania wa ngazi mbalimbali wanapata elimu na mafunzo ya ufundi ili kuwawezesha kujiajiri, kuajiriwa na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Akizungumza Agosti 7, 2025 alipowatembelea katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Profesa Mchome amesema lengo la VETA ni kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji ya soko na yanawasaidia wananchi katika maisha yao ya kila siku.

“VETA ni ya kila mtu. Leo nimetembelea banda letu kuangalia shughuli mbalimbali za maonesho haya yanayofanyika kila mwaka, lengo likiwa kuonyesha ubunifu na maendeleo tunayoyafanya. Tumeona hatua kubwa katika ubunifu, ikiwemo matumizi ya nishati ya umeme, na maonesho yajayo yatakuwa na ubunifu zaidi,” amesema Profesa Mchome.

Amesisitiza kuwa wadau wa VETA wanapaswa kwenda kwenye uzalishaji mkubwa wa bidhaa zinazobuniwa ili zitumike kwa wingi na kuchangia uchumi wa Taifa, akibainisha kuwa taasisi hiyo ni sehemu ya mchakato wa kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameweka fursa nyingi katika uchumi, lakini wanawake bado hawajazitumia ipasavyo.

“Kuna vyuo vya VETA, lakini wanawake wangapi wanachukua hatua ya kujifunza ujuzi wa ufundi? Namshukuru Mkurugenzi Mkuu wa VETA kwa kuhakikisha wanawake wanapata nafasi ya kujifunza ujuzi unaowakomboa kiuchumi,” alisema Senyamule.

Ametoa wito kwa wanawake kutumia fursa zilizopo, akieleza kuwa ujuzi wa ufundi ni maarifa ya haraka yanayoweza kuwasaidia kupata ajira au kujiajiri na kujipatia kipato.