Wakazi wa eneo la Gaza na mashuhuda wanasema makumi ya vifaru na magari ya kijeshi ya Israel yameingia katika wilaya kubwa ya makazi ya mji wa Gaza, katika siku ya pili ya mashambulizi ya ardhini ya Israel yenye lengo la kuteka eneo hilo.

Kanda za video zinaonyesha vifaru, tingatinga na wafanyakazi wenye silaha zikisonga pembezoni mwa Sheikh Radwan, kaskazini mwa jiji la Gaza.

Mawingu mazito ya moshi yanaweza kuonekana huku vikosi vya Israeli vikifyatua makombora ya risasi na mabomu ya moshi ili kuficha ujio wao.

Wilaya ya Sheikh Radwan ilikuwa makazi ya makumi ya maelfu ya watu kabla ya vita na inachukuliwa kuwa mojawapo ya maeneo yenye wakazi wengi zaidi wa jiji hilo.

Israel inasema lengo la mashambulizi yake katika mji wa Gaza ni kuwaachia huru mateka wanaoshikiliwa na Hamas na kuwashinda hadi wapiganaji 3,000 katika kile inachoeleza kama “ngome ya mwisho” ya kundi hilo – lakini operesheni hiyo imeshutumiwa kimataifa.