Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Zaidi ya vijana 50 kutoka vyuo vikuu na sekta mbalimbali wamepatiwa elimu ya mpiga kura ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi na kuchagua viongozi bora watakaoliongoza taifa kwa amani na maendeleo.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Kituo cha Kisheria na Usuluhishi (CRC) na kufanyika katika ukumbi wa TAMWA, Sinza Mori, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mradi wa Mafunzo hayo, Dkt. Gladness Munuo, amesema lengo ni kuwaelimisha vijana kuona umuhimu wa kujitokeza kupiga kura badala ya kudanganyika na mitazamo potofu inayoenezwa mitandaoni kwamba kupiga kura haina maana.

“Tumeona kundi kubwa la vijana ambao hawajawahi kupiga kura na hawaelewi umuhimu wake limeachwa kwa hiyo tunataka kundi hili liwe chachu ya kuwahamasisha wengine wajitokeze kupiga kura siku ya oktoba 29 .” amesema.

Dkt. Gladness ameongeza kuwa, kupitia mafunzo hayo na majadiliano yaliyofanyika, vijana wengi wameonyesha hamasa ya kuwa mabalozi wa kutoa elimu ya mpiga kura katika maeneo yao.

Aidha, amesema vijana wanapaswa kutambua kuwa baada ya miaka michache ijayo, baadhi yao wanaweza kuwa viongozi, hivyo ni muhimu kujifunza misingi ya uongozi na demokrasia mapema.

Mwezeshaji na Mwanaharakati Dkt Ave Maria, amesema ni wajibu wa vijana kujifunza sera za vyama na wagombea ili kufanya maamuzi sahihi wakati wa uchaguzi sio kubaki nyuma na kulalamika.

“Vijana lazima wajitambue na kuelewa nafasi yao katika nchi,kupiga kura ni haki na wajibu wa kila mmoja wetu kwa hiyo hampaswi kutumika kisiasa, bali muwe watu wenye msimamo na uelewa,” amesema .

Aliongeza kuwa vijana wanapaswa kutumia muda wao katika kujifunza na kujadili masuala ya msingi ya yanayowahusu wao na taifa badala ya kutumia muda mwingi kwenye mitandao au kufuatilia maisha ya wasanii na watu maarufu.

Ave amesema ni vyema washiriki wa mafunzo hayo wakaunda kikundi cha programu ya mafunzo hayo kuwa endelevu, hata ikibidi kufanyika kila mwezi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwafikia vijana wengi zaidi na uchaguzi mkuu wa mwaka 2030 waweze baadhi yao kujitokeza kugopmbe nafasi.

Kwa upande wake, Wakili Merryness Katabaro kutoka kituo hicho amesema elimu ya mpiga kura inawasaidia vijana kuelewa mabadiliko mapya ya kisheria kuhusu uchaguzi, ikiwemo haki ya mpiga kura kupiga kura sehemu yoyote nchini iwapo amehamisha taarifa zake kihalali.

“Sasa mtu anaweza kupiga kura popote nchini ilimradi amehamisha taarifa zake kutokana na sababu kama kazi, masomo au matibabu.

Pia wafungwa wenye vifungo visivyozidi miezi sita wanaruhusiwa kupiga kura,” amesema.