Ma Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana,Dk. Joel Nanauka, amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa za kiuchumi na kuwa tayari kushiriki shindano jipya la kitaifa la “Vijana Uchumi Challenge.”
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Aprili 12, 2026 Jijini Dar es salaam, Waziri Nanauka amebainisha kuwa shindano hilo si kwa ajili ya ushindani pekee, bali ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha uwezo wao wa kutoa fikra chanya zinazoweza kutatua changamoto za kijamii na kuchochea maendeleo ya taifa.
”Vijana wapo tayari kukamata fursa za kiuchumi kupitia shindano hili la Vijana Uchumi Challenge. Halilengi tu kupata mawazo bunifu, bali pia kutoa fursa kwa vijana kuonyesha uwezo wao wa kutoa fikra chanya kwa ajili ya nchi yetu,” amesema Nanauka.
Dk. Nanauka ameeleza kuwa kuanzishwa kwa shindano hilo rasmi ni hatua ya makusudi ya kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa nchi kupitia miradi na mawazo yao ya kibiashara.
Amesisitiza kuwa Rais Dk. Samia suluhu Hassan ameonesha uongozi wa mfano Kwa kuunda Wizara ya Vijana chini ya Ofisi yake ili masuala ya Vijana yaendee kupata uzito na uratibu wa karibu katika ngazi ya juu ya Serikali.

