Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga
Zaid ya vijana 200 mkoani Tanga wameshiriki mbio fupi maarufu kama jogging, wakitumia dakika 37.6 katika umbali wa kilomita 6.43, lengo likiwa ni kuhamasisha upigaji kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mbio hizo zilizoongozwa na mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, zilifanyika Jumamosi kuanzia jengo la Malikale la Urithi Tanga na kupita maeneo mbalimbali, kisha kumalizikia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (Bombo) walipofanya usafi wa mazingira.
Vijana wakimbiaji wakiwa na mwenyekiti wao, Abdallah Mselem, walisema kwa nyakati tofauti kuwa, mbio hizo ni ishara ya kuboresha afya zao na kujiepusha na magonjwa hasa yasiyokuwa ya kuambukizwa.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mselem alisema pamoja na kuboresha afya, vijana hao wameonesha kutambua, kuthamini na kuenzi mageuzi ya kimaendeleo katika sekta ya afya, hali inayothibitishwa kwa miongoni mwao kuwa wanufaika wakubwa.

Mmoja wa wakimbiaji hao, Asha Mndolwa, alisema kuwa mnufaika wa huduma bora ya damu salama aliyoipata, wakati akijifungua kwenye hospitali ya Bombo hivi karibuni.
Alisema, licha ya kujulishwa kuhusu ugumu wa upatikanaji damu ya ‘kundi lake’, lakini huduma hiyo ilipatikana na kumuwezesha kujifungua salama na kwamba yeye na mwanaye wanaendelea na afya njema.
Hivyo, alisema ipo haja kwa vijana wakiwemo wanufaika wa huduma kama za afya, kuwahimiza wananchi wenye sifa kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu huo, ili kuwapa viongozi wanaowajibika kwa umma.
Mkimbiaji mwingie, Hamis Mrisho, anasema pamoja na kukidhi matakwa ya mazoezi kwa afya kupitia mbio hizo, uboreshwaji huduma za Mama, Baba na Mtoto zimeinufaisha familia yake, na hivyo kumfanya ashawishike kuihimiza jamii kupiga kura ili kuwapata viongozi bora.

Alisema, mke wake Fatuma Jumaa, mkazi wa Duga Dampo, alijifungua huku kukiwa na hisia za kutakiwa kulipia gharama kubwa, hali iliyokuwa tofauti na uhalisia.
Kwa mujibu wa Mrisho, mkewe huyo hakudaiwa malipo kwa vile huduma za uzazi zinatolewa bure, hivyo fedha alizozitenga akazielekeza kwenye manunuzi ya lishe bora kwa Mama na Mtoto.
Naye Mkazi Mwang’ombe jijini Tanga, Popo Magao anayepata huduma endelevu za afya kwenye hospitali ya Bombo, alisema mbio na usafi uliofanywa na vijana hao, vinaakisi ukweli wa huduma bora ikiwemo kwa magonjwa ya kuambukizwa na yasiyokuwa ya kuambukizwa kwa wahitaji wakiwemo watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi.
Akizungumza katika kuhitimisha mbio na usafi huo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba alisema hatua iliyofikiwa na vijana hao ni kielelezo cha kuyatambua mafanikio ya Serikali katika kuwahudumia Watanzania, hivyo akawataka kuendelea kuuhimiza umma kupiga kura Oktoba 29, 2025.
“Tunapotoka hapa, tukawakumbushe wenzetu kila tutakapokuwa, kwamba tushiriki kupiga kura, kuwachagua viongozi watakaotufaa baada ya kuwa tumeshiriki na kusikiliza Ilani za Uchaguzi za vyama vyao,” alisema.
Alisema, Tanzania imerithi umiliki wa uongozi wa nchi unaotokana na Uchaguzi wa kidemokrasia, hivyo ni jukumu la kila raia kutumia haki yake kupiga kura.
