Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Darces Dalaam
TUME ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) imewaita vijana kuwekeza kwenye uchumi wa Buluu kupitia ubunifu katika mazao ya bahari ikiwemo mimea ya bahari, magamba ya chanza na mengineyo.
MKurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu alisema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye warsha ya wiki ya nchi za Nordic ambazo ni Dermark, Sweden, Norway na Finland.
Alisema vijana wasisite kuingia kwenye ubunifu wa mazao ya bahari na uchumi wa Buluu kwa sababu serikali inatambua suala hilo na ipo tayari kuwaunga mkono.
Alieleza kuwa serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali na kutoa fursa kwa vijana hivyo ikiwemo wajasiriamali wa zao la mwani kwa sababu serikali inafadhili zao hilo na wakulima wa zao hilo tayari wananufaika.
“Fursa zipo na taarifa za tafiti zipo ambazo zinawasaidia vijana kutoka kwenye tafiti kwenda kwenye uwekezaji, pia tunapokea mawazo mapya au yanayotakiwa kuboreshe kwa hiyo vijana wenye mawazo walete tujadiliane na tunashauri pia,” alisema Nungu.

Alibainisha kuwa nchi za Nordic zinamchango mkubwa katika kuwezesha vijana katika masuala ya ubunifu na ujasiriamali.
“Hivi karibuni Norway na Sweden kupitia Costecha wamefadhili utafiti wa mabadiliko ya tabia ya nchi, sasa kwenye uchumi wa Buluu ni eneo ambalo serikali inaliangalia sana hivyo serikali tunawashukuru kwa kuja na huu mradi wa kukusanya mawazo bunifu na kuangalia bunifu zilizopo kwa wajasiriamali wa mzao ya bahari,” alisema.
Dk Nungu alisema serikali imekuwa ikiunga mkono suala hilo kwa kushirikiana na serikali ya Zanzibar ikiwemo kuwagawia wajasiriamali na wakulima wa zao la mwani boti ndogo kwa ajili ya kufanya shughuli zao.
Alieleza wakati mwingine changamoto iliyopo ni watu kuona ubunifu ni matumizi ya teknolojia pekee hivyo serikali inatambua hilo na ubunifu kwa serikali kila kitu kuna ubunifu wa bidhaa na mifumo.
Kwa upande wa Balozi wa Sweden nchini, Charlotta Macias alisema wiki hiyo ya Nordic ni ishara ya uendelevu wa ushirikiano katika kukuza mawazo bunifu ya mazao ya bahari na ushirikiano baina ya Tanzania na Sweden, Dermark, Finland na Norway.
Alisema wiki hiyo pia inalenga kuwaunganisha watu kwa ajili ya kubadilishana maarifa, kuhamasisha suluhisho wa utunzaji wa bahari, na kuharakisha maendeleo kuelekea mustakabali endelevu zaidi.
Alibainisha kuwa wiki ya Nordic inalenga kuwaleta watu pamoja kubadilishana maarifa,kuhamasisha ubunufu na kuharakisha maendeleo kuelekea maisha endelevu.
“Katika kuinua biashara za uchumi wa buluu lazima tuwe na wazo la ubunifu linaloangazia bahari kwa sababu kila pumzi ya pili tunayopumua inatoka baharini. Bahari huzalisha asilimia 50 ya oksijeni tunayopumua pia bahari inadhibiti hali ya hewa chafu,inatoa ajira na inasaidia kuendeleza uhai wa viumbe hai,” alisema Balozi Macias.
Aliongeza “lakini sote tunajua kuwa bahari ziko hatarini kutokana na uchafuzi wa mazingira, uvunaji wa viumbe bahari upita kiasi, na taka za plastiki ambazo haziozi sasa kwenu ninyi waanzilishi wa miradi ya ubunifu wa bahari mnapaswa kuthibitisha kuwa ubunifu si maneno matupu bali mnatoa pia njia za kushughulikia changamoto hizo za kimataifa na kupata suluhisho litakalosaidia mazingira ya bahari yanakuwa salama,” alisema.
Pia alisema dunia inahitaji mabadiliko katika utunzaji wa bahari hivyo wahakikishe wakati wanabuni mawazo yao ya biashara wahakikishe wanabuni mawazo yatakayotoa suluhisho endelevu kwa jamii katika utunzaji wa bahari.
Alieleza kuwa nchi za Nordic zimekuwa mstari wa mbele kwa muda mrefu katika kwa wajasiriamali kwa kutoa uongozi wa kimazingira, na suluhisho za kisasa.
Aidha, alitoa wito kwa wajasiriamali hao kuhakikisha wanajitoa katika kuzuia matumizi ya chupa za plastiki katika maeneo ya fukwe pamoja na kushiriki kufanya usafi kwenye fukwe kwa ajili kutunza kwa vizazi vijavyo
Naye, mmoja wa wajasiriamali wa mazao ya bahari, Fahia Ismail alieleza kuwa kwenye uchumi wa bluu kuna fursa nyingi zinazotokana na mazao ya bahari ikiwemo biashara za ujasiriamali ukulima wa mwani ambapo zinazalisha bidhaa mbalimbali.
Alisema licha ya uwepo wa fursa hizo lakini bado kuna changamoto ya wawekezaji na wafanyabiashara wa kutosha jambo ambalo linasababisha watu kushindwa kufanya uvumbuzi au ubunifu wa kupata bidhaa mpya.
Fahia alisema kwenye sekta ya uvuvi, wavuvi wengi wanajihusisha kwenye uvuvi mdogo mdogo na si uvuvi wa bahari kuu ambao kuna fursa.
“Pia kuna utalii wa bahari ambao kwa nchi yetu bado ni mdogo watu wengi wameshazoea kuwa tukiongelea utalii wa bahari na uchumi wa bluu tunaongea Zanzibar lakini hata Tanzania Bara ina fukwe nyingi za kuvutia na watu hawajawahi kufika huko.Kuna fursa ya kutengeneza hereni na mikufu kutumia magamba ya samaki lakini watu hawajabuni kutumia mazao ya bahari kutengeneza vitu vipya na kubaki kufanya shughuli ambazo tayari watu wanafanya,”alisema Fahia