Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana leo mjini Brussels katika juhudi za kutafuta majibu ya pamoja dhidi ya azma ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kukitwaa kisiwa cha Greenland.
Rais Trump alikuwa ametangaza kuziwekea ushuru wa asilimia 10 bidhaa kutoka kwa washirika kadhaa wa Ulaya kuanzia Februari Mosi, lakini alibadilisha mawazo yake siku ya Jumatano.
Mabadiliko hayo ya Trump aliyatangaza mjini Davos Uswisi, wakati akihutubia Jukwaa la Kimataifa la uchumi, na kusema kuwa kuna mfumo mpya wa makubaliano na NATO kuhusu usalama katika kanda ya Aktiki bila Marekani kutumia nguvu kuchukua Greenland.
Hata hivyo, bado kulikuwa na maswali mengi ambayo hayajajibiwa kuhusu maana ya makubaliano hayo ya Greenland.
Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, amekaribisha uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kuachana na vitisho vya kutwaa Greenland kwa nguvu kutoka kwa mshirika wake Denmark, akikiita kitendo hicho “njia sahihi ya kufuata.”



