Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imevitaka vyama vya siasa kuwasilisha kwa wakati taarifa za gharama walizotumia katika Uchaguzi Mkuu ili kuimarisha uwazi na demokrasia nchini.
Akizungumza leo Machi 10, 2026 jijini Dar es Salaam, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ally Ahmed, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha utekelezaji sahihi wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
Amesema hayo wakati wa mafunzo ya namna ya kujaza fomu za gharama za uchaguzi katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa vyama vya siasa pamoja na maafisa wa ofisi hiyo, kwa lengo la kutoa elimu kuhusu sheria hiyo.

Aidha, amewashukuru viongozi wa vyama vya siasa kwa ushirikiano wao wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita uliofanyika Oktoba 29, ambapo vyama mbalimbali vilishiriki kwa amani na kufuata misingi ya Katiba ya nchi.
“Sheria ya gharama za uchaguzi inavitaka vyama vya siasa na wagombea kujaza na kuwasilisha fomu zinazoonyesha vyanzo vya fedha walizotumia katika kampeni kabla na baada ya uchaguzi. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha fedha zinazotumika katika siasa zinatoka katika vyanzo halali na kuepuka ushawishi usiofaa kutoka nje ya nchi au matumizi ya fedha haramu,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa kuwepo kwa ukomo wa matumizi ya fedha kunasaidia kuweka usawa kati ya vyama vikubwa na vidogo na hivyo kuimarisha demokrasia.
Amesisitiza kuwa lengo la sheria hiyo si kuzuia shughuli za vyama vya siasa, bali ni kuhakikisha kila chama kinapata nafasi sawa katika kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia.
“Ofisi ya Msajili imeendelea kutoa elimu kwa viongozi wa vyama ili kuongeza uelewa wa sheria hiyo, hasa baada ya kubainika kuwa baadhi ya vyama bado vinakabiliwa na changamoto katika kujaza fomu za gharama za uchaguzi,” amesema.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu, amesisitiza umuhimu wa viongozi wa vyama vya siasa kujaza kwa usahihi fomu za taarifa za gharama za uchaguzi kama inavyotakiwa kisheria.
Amesema katika kila mwaka wa uchaguzi, vyama vya siasa vinapaswa kuwasilisha hesabu na taarifa za matumizi ya fedha zilizotumika katika kampeni ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa kidemokrasia.
“Mafunzo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa yanawaleta pamoja makatibu wakuu wa vyama, wahusika wa uchaguzi pamoja na wadhamini ili kuwajengea uwezo wa kujaza ipasavyo fomu za gharama za uchaguzi kabla ya kuwasilishwa kwa Tume ya Uchaguzi,” amesema Khatibu.
Amesema awali kulikuwa na changamoto ya kutoeleweka vizuri kwa sheria hiyo, lakini mafunzo ya mara kwa mara yameanza kusaidia vyama kuelewa wajibu wao.

Amefafanua kuwa sheria ya gharama za uchaguzi inalenga pia kuweka usawa kati ya vyama vya siasa kwani baadhi vina uwezo mkubwa wa kifedha huku vingine vikiwa na uwezo mdogo.
“Sheria hiyo inasaidia kudhibiti matumizi makubwa ya fedha katika kampeni na kuhakikisha fedha zinazotumika zinatoka katika vyanzo halali ili kuepuka fedha chafu au kutoka nje ya nchi ambazo zinaweza kuathiri demokrasia,” amesema.
Khatibu amewataka viongozi wa vyama kujaza fomu hizo kwa umakini na uaminifu mkubwa kwa kuambatanisha vielelezo vinavyoonyesha matumizi halisi ya fedha.
Ameonya kuwa taasisi mbalimbali za serikali zina jukumu la kuchunguza taarifa hizo na kuchukua hatua za kisheria iwapo kutabainika udanganyifu, huku akisisitiza kuwa uwazi na ukweli ni msingi muhimu katika kulinda mfumo wa demokrasia nchini.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Esther Thomas, amesema sheria ya gharama za uchaguzi ni muhimu katika kipindi hiki ambapo kumekuwepo na changamoto ya ubadhilifu wa fedha katika shughuli za kisiasa.
Amesema sheria hiyo, ambayo sasa inatumika kwa mara ya pili, inalenga kuweka usawa kati ya vyama vya siasa ili kuzuia vyama au wagombea wenye uwezo mkubwa wa kifedha kutumia fedha kupita kiasi wakati wa kampeni.
“Utaratibu huo unasaidia pia kutoa nafasi kwa vyama vidogo kushiriki katika uchaguzi kwa ushindani wa haki bila kuzidiwa na vyama vyenye uwezo mkubwa wa kifedha,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, amesema warsha hiyo ni muhimu na imekuja wakati muafaka kwani imewaongezea uelewa.
“Kwetu sisi vyama vya siasa tumepokea kwa furaha jambo hili na tunaipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuandaa mafunzo haya. Sheria ya gharama za uchaguzi inatuhitaji kuonesha vyanzo na gharama ambazo chama kimetumia,” amesema Doyo.




