Kwa wiki mbili sasa sijaonekana katika safu hii. Niwie radhi msomaji wangu sikuchagua kutokuwapo, bali kutokana na kazi nzito ya kuchunguza magendo mpakani huko Tunduma, ilinipasa nisiwe mshika mawili. Leo nimerejea. Salamu za heri huwa hazichachi. Msomaji wangu nakutakia heri ya Krismasi na Mwaka Mpya, 2017, nikitaraji mwaka huu pamoja na magumu yake utaumaliza salama, na mwakani utajipanga sawa sawa.

Sitanii, tunaendelea na mageuzi ndani ya chumba cha habari. Kubwa zaidi tunataka gazeti hili kuwa na habari nzito za kiuchunguzi na zenye maslahi kwa umma. Ni kwa mantiki hiyo hata safu zilizo nyingi tutazipunguza kuwa nusu ukurasa. Tunapenda wachangiaji wetu watoe ujumbe kwa maneno machache, lakini yenye mshindo mkuu.

Leo nazungumzia nia ya Serikali kutovipatia matangazo vyombo vya habari binafsi. Tusipoangalia linaweza kuua demokrasia nchini. Naomba kutangaza maslahi kuwa namiliki kampuni inayojihusisha na masuala ya habari – Jamhuri Media Limited.

Baada ya kutangaza maslahi nieleze kuwa Serikali kupitia mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2016/2017 imetangaza nia ya kutotangaza na vyombo vya habari binafsi. Sheria ya Huduma za Habari (MSA) iliyotungwa mwaka huu kifungu cha 5(l) kinaipa Idara ya Habari (MAELEZO) mamlaka ya kuratibu matangazo yote ya Serikali.

Lakini wakati sheria hii haijaanza kufanya kazi, tayari utekelezaji umeanza serikalini. Baadhi ya taasisi za umma zilizokuwa zinavipatia matangazo vyombo vya habari binafsi tukiwamo sisi, tayari zimesitisha matangazo kwa maelekezo ya baadhi ya mawaziri. “Ikiwezekana mwambieni Mhe. Rais Magufuli. Mnafanya kazi kubwa, ila tumeelekezwa tusiwape matangazo,” mmoja wa maafisa wanaosimamia matangazo ameniambia.

Ni kutokana na kauli hii Jumamosi iliyopita tuliungana na  Mwenyekiti (mstaafu) wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, Katibu wa Jukwaa, Neville Meena, na mimi –  Makamu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, tukaenda Star TV asubuhi kueleza kutokuridhishwa kwetu na mpango huu wa Serikali.

Sitanii, hatupingi mpango huu kwa sababu tunataka kujinufaisha, la hasha, bali kutokana na ukweli mchungu. Kwamba vyombo vya habari binafsi vimekuwa mstari wa mbele kufichua uozo katika nchi hii, jambo ambalo si siri. Gazeti hili la JAMHURI limefichua wizi wa mafuta bandarini kwenye flow meters hadi likapongezwa na Rais Dk. John Magufuli. Kwa kufichua mchezo huo, limesaidia kuokoa mabilioni ya shilingi.

Gazeti hili la JAMHURI limeripoti habari za Kampuni ya Lake Oil kukwepa kodi katika mafuta ya ‘transit’, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) ikachunguza na kubaini kuwa ni kweli Lake Oil ilikwepa wakapigwa faini na wakalipa Sh bilioni 8.5. Tumefichua upotevu wa mamilioni uliokuwa ukifanywa na Kampuni ya TBL.

Kama hiyo haitoshi, wiki iliyopita gazeti hili limefichua njia 320 za panya katika mpaka wa Tunduma zinazolipotezea taifa wastani wa Sh bilioni 100 kwa mwaka. Serikali ikizifanyia kazi habari hizi, nina uhakika itakusanya mabilioni ya kodi yanayopotea. Sijaona gazeti la Serikali likifanya kazi kama hii. Vyombo vya habari binafsi ndivyo vilivyofanya kazi hii ya kupigiwa mfano.

Sitanii, kazi za vyombo vya habari binafsi zinaisaidia zaidi Serikali kuliko vyenyewe vinavyonufaika. Tukifichua wakwepa kodi, haturejeshewi hata senti tano kutushukuru kwa kazi tuliyoifanya. Gharama za kufanya habari za uchunguzi ni kubwa. Hakuna gazeti linaloweza kujiendesha kwa kutegemea mauzo ya gazeti. Niliamini kuwa Serikali kama mnufaika mkuu wa kazi za vyombo vya habari binafsi, ilipaswa kutetea vyombo hivi kuendelea kupewa matangazo vikazidi kufichua uozo.

Inawezekana Rais Magufuli amepewa taarifa zisizo sahihi kwa sasa. Tangu ameingia madarakani amefanyia kazi habari nyingi zilizotokana na vyombo vya habari binafsi. Inawezekana mafisadi wanamzunguka na sasa wamepata kamba ya kuvinyongea kwa kuvinyima matangazo. 

Chonde chonde Rais Magufuli, naomba uingilie kati kusitisha mpango huu maana hauna maslahi kwa Taifa. Kuua vyombo vya habari binafsi ni sawa na kuzima taa za gari usiku gizani wakati unaendesha kwa kasi ufike haraka katika safari ya viwanda, matokeo unayafahamu.

By Jamhuri