Na John Walter, JamhuriMedia, Babati

Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8,2026 Halmashauri ya Wilaya ya Babati imefanya shughuli za kijamii kwa kupanda miti na kugawa misaada mbalimbali katika Kituo cha Kulelea Wazee kilichopo Sarame, Kata ya Magugu.

Shughuli hiyo imeandaliwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii chini ya uongozi wa Mkuu wa Idara hiyo, January Bikuba, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya wanawake duniani pamoja na kuonesha mshikamano na makundi maalum katika jamii.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Bikuba amesema zoezi la upandaji miti linalenga kuboresha mazingira ya kituo hicho pamoja na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuhimiza utunzaji wa mazingira nchini.

“Tunapoadhimisha wiki ya wanawake duniani, tumeona ni vyema kuunganisha maadhimisho haya na vitendo vya huruma na utunzaji wa mazingira. Hii ni sehemu ya kumuunga mkono Rais wetu katika ajenda ya mazingira na maendeleo endelevu,” amesema Bikuba.

Aidha, amesema wametoa misaada mbalimbali kwa wazee hao ili kusaidia mahitaji yao ya kila siku, akibainisha kuwa wazee ni hazina ya taifa kwani waliipambania nchi kwa namna moja au nyingine na wanastahili heshima na uangalizi maalum.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii anayehudumu katika kituo hicho, Maige Jackson, amesema serikali imeweka mipango madhubuti ya kuwahudumia wazee kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Wazee ya mwaka 2023.

Ameeleza kuwa hali ya huduma katika kituo hicho ni nzuri, ikiwemo huduma za afya, malazi na chakula.

Ameongeza kuwa hivi karibuni wazee wa kituo hicho walipatiwa bima ya afya kwa wote bure na serikali, hatua inayosaidia kuboresha zaidi ustawi wao.

Wazee wanaoishi katika kituo hicho wameishukuru serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwa kuwakumbuka na kuendelea kuwajali, wakisema hatua hiyo inawapa faraja na kuwafanya wajione kuwa sehemu muhimu ya jamii.

Naye Diwani wa Kata ya Magugu, Mheshimiwa Stanley Charles, amesema mwanamke ni nguzo ya maendeleo na chachu ya mafanikio katika jamii.

Ametoa mfano wa Samia Suluhu Hassan akisema ameonesha kuwa wanawake wanaweza kushika nafasi za juu za uongozi na kuleta mabadiliko chanya.

Kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2026 inasema: “Haki na usawa kwa wanawake na wasichana, msingi jumuishi kuelekea dira ya taifa letu 2050,” ikisisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia kama nguzo ya maendeleo ya taifa.