Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dodoma

Taasisis za WAJIBU na Policy Forum, wamezindua mradi wa raia makini kwa kuwajengea uwezo wanahabari na AZAKI katika suala la uwajibikaji kwenye usimamizi wa fedha za umma ili waweze kushiriki kikamilifu katika kudai uwazi na uwajibikaji.

Akizungumza katika mkutano huo wa siku tatu unaofanyika jijini Dodoma Mkurugenzi mtendaji wa Taaaisi ya WAJIBU , Ludovic Utouh, amesema lengo kuu la mradi huo ni kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo,waandishi, AZAKI na wananchi katika usimamizi wa fedha za umma katika makusanyo na matumizi.

Utouh amesema fedha za umma hazina mambo ya siasa zimenyooka tu ,kazi yake ni kuwaletea wananchi maendeleo na kuhakikisha pesa zinazo patikana zinatumika kama zilivyoainishwa.

“Tunaimani mradi utaimarisha,mashirikianano kati ya AZAKI,vyombo vya habari na Wananchi kwa kushirikiana na viongozi kupitia majukwaa rasmi ya majadiliano katika ngazi ya kitaifa na wilaya.

Hii italeta fursa zaidi Kwa wananchi ,kushiriki katika maamuzi na usimamizi wa fedha za umma kuelezea mradi ambao kwa kifupi tunauita “ Raia Makini Project” (mtu anayejielewa, mshiriki, mfuatiliaji, muwajibikaji, na mchukua hatua” amesema.

Amedai mradi huo umeandaliwa , ili kuwe na uwajibikaji bora katika usimamizi wa fedha za umma ni lazima kuwa na wananchi ambao wanataarifa na uelewa mpana wa maswala ya uwajibikaji ambao wataweza kushirikiana na Serikali katika kusimamia fedha za umma, kudai uwajibikaji pamoja na kupinga rushwa.

“Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Umoja wa Ulaya (European Union Commission) kwa kuonyesha imani na dhamira ya dhati ya kuimarisha utawala bora, uwazi na uwajibikaji nchini Tanzania kupitia mradi huu”Amesema.

Utouh amesema maudhui ya mradi unalenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa fedha za umma.

Amesema mradi utaandaa na kusambaza taarifa muhimu kwa lugha rahisi kuhusu usimamizi wa fedha za umma, huku ukiwawezesha wadau wa uwajibikaji kuhamasisha uwazi na uwajibikaji wa Serikali.

“Hili litaleta fursa zaidi kwa wananchi kushiriki katika maamuzi na kuimarisha uwajibikaji ndani ya nchi.

Mradi huu una malengo mahususi matatu yanayohusiana kwa karibu, kama ifuatavyo:Kuzalisha na kusambaza taarifa kwa lugha rahisi kuhusu usimamizi wa fedha za umma, kwa ajili ya kuwawezesha wananchi na wadau wasio wa serikali kushiriki kwenye mijadala ya umma na midahalo ya sera, na kushawishi mageuzi ya sheria na kuimarisha wa mifumo.

Kuimarisha uwezo wa wadau wa uwajibikaji kuhusu usimamizi wa fedha za umma ili waweze kushiriki kikamilifu na kwa ufanisi katika kudai uwazi na uwajibikaji kutoka kwa wenye mamlaka katika ngazi ya kitaifa na za wilaya.

Kukutanisha asasi za kiraia, vyombo vya habari, na wananchi ili kushirikiana na viongozi wa maamuzi katika kuhamasisha uwazi na uwajibikaji kwenye usimamizi wa fedha za umma, ukusanyaji wa rasilimali za ndani, na mapambano dhidi ya rushwa.

Wanufaika wa Mradi: Mradi huu ni wananchi, Vyombo wa Uangalizi, Bunge na Baraza la Uwakilishi Zanzibar, Vyombo vya Habari, AZAKI, Wizara, Idara na Mawakala wa Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa, TAKUKURU, na ZAEKA.

Mradi huu ni wa wananchi sote tukawe ni jukwaa la mabadiliko chanya katika usimamizi wa rasilimali za umma kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.

Kwa ushirikiano wa AZAKI, Serikali, Vyombo vya Habari na Wananchi, tunaweza kuleta mageuzi yenye tija na usawa nchini katika kumjenga raia makini na uwajibikaji utakuwa wa kuridhisha.


Mwakilishi kutoka Afisi ya Mdhibiti na Mkugaguzi Mkuu ( CAG) Zanzibar, Mkarugenzi wa Ukaguzi wa Mifuko ya TEHAMA, Juma Mohamed Juma amesema mradi huo ulioanzishwa na WAJIBU na Policy forums,unalengo la kuisaidia Serikali katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma zilizopelekwa kwa Wananchi.

Amesema anazipongeza taaaisi hizo kwakuanzisha mradi huo wenye lengo la kuimarisha utawala bora nchini ikiwemo pande zote mbili Zanzibar na Bara.

Amesema kwa upande wao, wataweza kuyachukua yale yote yaliyojadiliwa na kuyapeleka katika afisi yao .

“Ushirikiano wenu utakuwa ni mkubwa sana , kwasababu utahakikisha fedha zinazo kusanywa zinatumika katika malengo yaliyo kusudiwa “amesema.

Mwakilishi wa CAG Bara ,Naibu mkaguzi mkuu Wendy Massoy amesema lengo la mradi huo ni kuwa na raia makini,ambapo mwananchi atawezeshwa kufahamu jinsi ya kufuatilia fedha za umma.

Wendy amesema katika ofisi ya CAG mradi huo utasadia kuonyesha jinsi gani ,kazi ya CAG ina boreshwa, kwasababu ukaguzi wa sasa ni shirikishi na mdau mkubwa ni mwananchi sasa akielewa atatusadia kama ofisi.

Mkurugenzi wa Policy forums Semkae Kilonzo amesema lengo la mradi huo ni kuwashirikisha wadau wote ,ili kuona wanaunganisha nguvu katika suala la uwajibikaji wa fedha za umma

“Nafarijika sana kuona tupo timu moja yenye nguvu , tunaweza kufanya kazi pamoja baada ya kujengewa uwezo katika masuala ya uchechemuzi”Amesema

Zaidi ya washiriki 60 kutoka vyombo vya mbalimbali vya habari ,AZAKI na viongozi wa Serikali wameshiriki mafunzo hayo.